Na Mwamdishi Wetu,Dodoma
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa ufanisi katika ukusanyaji wa mapato bila kuvutana na wananchi na matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Akizungumza wakati wa semina ya mafunzo kuhusu mfumo wa usimamizi wa kodi za ndani (IDRAS), mfumo wa Forodha TANCIS na mfumo wa uondoshaji mizigo Bandarini iliyotolewa kwa Kamati hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiongozwa na Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mashimba Ndaki amesema kazi nzuri inayofanywa na TRA inaipeleka Tanzania kwenye kujitegemea kiuchumi kwa kiasi kikubwa.
Amesema kila wakati TRA inapopewa malengo na Serikali imekuwa ikiyavuka na kutolea mfano makusanyo ya kodi ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo TRA imekusanya kiasi cha Sh. Trilioni 10.65 sawa na asilimia 107.49 ya lengo la kukusanya Sh. Trilioni 9.91kiwango ambacho ni kikubwa kuwahi kukusanywa kwa kipindi kama hicho.

Amesema mafanikio ya makusanyo hayo yamechagizwa na matumizi ya mifumo pamoja na ukaribu baina ya TRA na walipakodi ambapo wamekuwa wakiwapatia elimu ya kodi na kukusanya kodi bila kuvutana nao.
“Tunawapongeza sana kwa utendaji kazi mzuri mnaofanya na hii inatuonyesha kuwa tutatimiza makadirio ya Bajeti yaliyowekwa na Serikali ya kutaka Tanzania ijitegemee kwa asilimia 75 kwa mapato ya ndani” amesema Mhe. Ndaki.
Amesema semina waliyopewa na TRA kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijitali ya IDRAS, TANCIS na uondoshaji mizigo Bandarini yamewaongezea uelewa huu ya kazi za TRA hali itakayowawezesha kufuatilia kwa karibu na kusimamia masuala yanayohusiana na ukusanyaji wa mapato.
Amesema watakuwa mabalozi wa mifumo hiyo ili kuhakikisha kila kinachotakiwa kukusanywa kinakusanywa kwa wakati ili kuisaidia nchi kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Tunapoona barabara zinajengwa ni kodi, tunapoona shule zinajengwa ni kodi na pale tunapoiomba Serikali itekeleze .miradi ya elimu, afya na maji hizo nazo ni kodi hivyo kila mwananchi anapaswa kutimiza wajibu wake kwa kulipa kodi” Mhe. Ndaki.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema TRA inaendelea kujiimarisha kimifumo ili kurahisisha ulioaji kodi na kuwa wametoa semina hiyo ya mafunzo kwa Wabunge ili kuwawezesha kuwa mabalozi wazuri wa ukusanyaji wa mapato.
Mwenda amesema mifumo ya kodi kwa kiasi kikubwa imeboresha utawala wa kodi na kupunguza kuonana kwa watumishi wa TRA na walipakodi pamoja na kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa kodi.

Amesema kuwa idadi ya Walipakodi nchini imefikia 9,000,000 ikihusisha Waajiriwa, Wafanyabiashara na wawekezaji ambapo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027 TRA imesajili Walipakodi wapya zaidi ya 447,000 hali iliuochagizwa na msamaha wa kodi kwa biashara mpya.
Kamishna Mkuu huo ameihakkoshia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuwa TRA itaendelea kuwezesha biashara nchini na kutoa huduma bora kwa walipakodi kwa kuwatembelea, kuwasikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.

Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Esther Matiko amesema semina ya mafunzo waliyopatiwa imewawezesha kujua zaidi kuhusu TRA na kueleza.kuwa mipango ya Mamlaka hiyo kufunga Scanner za ukaguzi wa mizigo kwenye mipaka yote itasaidia kuboresha zaidi huduma za kodi na kudhibiti mapato.
Amesema kutokuwepo kwa Scanner kwenye baadhi ya mipaka ikiwemo Sirali kunaweka mwanya wa upotevu wa mapato hivyo udhibiti ukiwekwa kodi itaokolewa.
Mhe. Matiko ameipongeza TRA kwa kuweka utulivu katika ukusanyaji wa mapato na kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi.


