REA YASHINDA TUZO ZA TAASISI BORA ZA UMMA DUNIANI

📌Yapongezwa kwa kuboresha maisha ya Wananchi Vijijini

Na Mwnadoshi Wetu, Dubai

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeibuka miongoni mwa washindi wa tuzo za Dunia za Utumishi wa Umma (World Public Service Awards, 2026), zilizolenga kutambua mchango wa Taasisi na Mashirika ya Umma unaotokana na huduma zinazotolewa na namna zinavyoboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo zilizofanyika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Dubai, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi, Advera Mwijage kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Hassan Saidy, amesema kuwa wamepokea kwa furaha tuzo hiyo na kwamba tuzo hiyo inakwenda kuwa chachu ya kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuboresha maisha ya wananchi vijijini.

“Tuzo hii kwetu ina maana kubwa sana na imekuwa kama deni kwetu kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi kuhakikisha wananchi vijijini wanaendelea kupata nishati bora, salama, endelevu na nafuu kwa maendeleo yao na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla,” amesema Mhandisi, Mwijage.

Mhandisi, Mwijage amesema kuwa mafanikio yaliyofikiwa yasingeweza kufikiwa kama Serikali isingetoa fedha kwa wakati kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini.

“Tungependa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa wakati pamoja na Wabia wa Maendeleo wanaoshirikiana na Serikali katika kufadhili miradi mbalimbali tunayotekeleza. Kwa pamoja tumeweza kuyagusa maisha ya wananchi vijijini na matokeo yake yamefanya tuweze kutambulika Kitaifa na Kimataifa kwa kupatiwa tuzo mbalimbali ikiwamo tuzo hii,” ameongeza, Mhandisi Mwijage.

Ameongeza kuwa, REA itaendela kutekeleza na kubuni miradi inayolenga kuendelea kuboresha maisha ya wananchi vijijini kupitia sekta ya nishati.