DAWASA YAREJESHA MAJI KIKONGO BAADA YA MIAKA MIWILI

Na Mwandishi Wetu,Pwani

Wakazi takribani 1,500 wa Vijiji vya Lupunga, Videte na Kwa Mkino, Katika Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, wameanza kupata huduma ya majisafi baada ya kukosekana kwa huduma hiyo kwa kipindi cha miaka miwili, iliyosababishwa na kuharibika kwa pampu katika kituo cha kusukuma maji Mpera.

Meneja wa DAWASA Kibaha, Mhandisi Barnabas Taligunga, amesema Mamlaka imefunga pampu mpya katika kituo hicho baada ya kubaini changamoto iliyokuwa ikiwakabili wananchi kwa muda mrefu.

“Tumetambua shida waliyoipitia kwa muda mrefu ya kukosa maji kwa muda mrefu na kutumia maji ambayo vyanzo vyake havikiwa salama, DAWASA imechukua jitahada za makusudi kurejesha huduma kwa wananchi kwa kununua na kufunga Pampu mpya yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milion 6.5 ili waendelee kupata huduma waliyoikosa kwa muda mrefu,” amesema Taligunga.

Amesema kazi ya kufunga pampu hiyo imekamilika na wananchi wameanza kupata maji kupitia kituo hicho, ambacho hupeleka maji kwenye tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 25,000 kwa ajili ya usambazaji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupunga, Hashim Ndolwa, ameishukuru DAWASA kwa kurejesha huduma hiyo, akisema wananchi walikuwa wamepitia kipindi kigumu kutokana na ukosefu wa maji salama.

“Baadhi walikuwa na visima binafsi, lakini maji yake hayakuwa safi na hayakutosha. Hatua hii inaleta faraja kubwa kwa wananchi,” amesema Ndolwa.

Mkazi wa Videte, Mwanahawa Yona, amesema ukosefu wa maji ulikuwa umeathiri maisha yao, huku akieleza kuwa kurejeshwa kwa huduma hiyo kumewapa faraja na matumaini ya kupata maji salama kwa uhakika.

“Tunashukuru kwa sababu furaha imekuja baada ya kuanza kupata majisafi na salama. Tunatumaini yatapatikana kwa uhakika,” amesema Yona.