Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri wa Majini, kitakachokuwa kitovu cha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji kwa nchi za Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika.
Chuo hicho kinatarajiwa kuwawezesha wataalamu wa sekta ya uchukuzi kupata ujuzi unaohitajika katika kuimarisha huduma za bandari, usafirishaji wa mizigo na abiria, usalama wa majini na ushindani wa biashara katika soko la kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Shirika la Bahari la Kanda ya Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini utakaofanyika Oktoba 15, 2026.
Alisema Tanzania itafanya ujenzi huo kwakushirikiana na nchi wanachama katika kuendeleza mpango huo ambapo chuo hicho, kinachotarajiwa kuhudumia nchi wanachama wa shirika hilo, kitakuwa sehemu muhimu ya kujenga uwezo wa wataalamu wa Afrika katika sekta ya usafiri wa majini.

“Serikali imeendelea na mchakato wa kuanzisha chuo hicho kwa kutambua kuwa maendeleo ya sekta ya uchukuzi hayawezi kutegemea uwekezaji katika miundombinu pekee bila kuwa na wataalamu wenye ujuzi unaohitajika,”alisema Kihenzile.
Aliongeza kuwa chuo hicho kitasaidia kuimarisha utafiti na ubunifu, pamoja na kuandaa kizazi kipya cha wataalamu watakaokidhi mahitaji ya sekta hiyo katika ukanda wa Afrika.

Katika hatua nyingine Kihenzile alisema bandari ya kuwa Tanzania ina nafasi muhimu katika kurahisisha biashara kati ya nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini pamoja na masoko ya kimataifa kutokana na jiografia yake na uwepo wa bandari zinazohudumia nchi za ndani zisizo na mwambao wa bahari.
Alisema bandari ya Dar es Salaam ilitajwa kuwa lango muhimu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zikiwamo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda.
“Takwimu zinaonesha kiasi cha shehena iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kiliongezeka kutoka takribani tani milioni 14.1 mwaka wa fedha 2021/22 hadi tani milioni 25.7 mwaka wa fedha 2025/26.

“Ukuaji huo unaonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari, mifumo ya kisasa ya kuhudumia mizigo na huduma zinazorahisisha biashara katika ukanda huo,”alisema Kihenzile.
Alisema ufanisi wa bandari hiyo si suala la Tanzania pekee, bali ni jambo linalogusa muunganiko wa uchumi, ushindani wa kibiashara na maendeleo ya nchi zinazotegemea huduma zake.


