Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaa.
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Shirika la Bahari la Kanda ya Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA)utakaofanyika Oktoba 15, 2026, katika Hoteli ya Johari jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alisema mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na takribani mawaziri 26 zinazohusika na masuala ya uchukuzi na usafirishaji kutoka nchi wanachama hasa katika sekta ya bahari.

Alisema miongoni mwa nchi zilizotajwa ni Tanzania, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Burundi, Botswana, Malawi, Angola, Comoro, Djibouti, Misri, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Somalia, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Sudan na Zimbabwe.
“Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, zikiwamo Umoja wa Afrika, Benki ya Maendeleo ya Afrika na mashirika yanayohusika na usalama, viwango na maendeleo ya usafiri wa majini,”alisema Kihenzile.

Alisema mkutano huo unalenga kujadili namna ya kuimarisha biashara kwa kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya meli katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Alisema mkutano huo ni muhimu kuwakuwa usafirishaji wa majini una nafasi kubwa katika uchumi wa dunia, huku zaidi ya asilimia 90 ya biashara ya nje ya nchi nyingi ikitegemea usafiri wa baharini.
“Zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya bidhaa duniani kwa ujazo husafirishwa kwa njia ya bahari, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuboresha bandari na mifumo inayounganisha maeneo ya uzalishaji na masoko.

“Ktokana na hali hiyo, Tanzania imeeleza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa majini ili kupunguza vikwazo vya biashara, kuongeza uwekezaji na kukuza ajira,”alisema Kihenzile.
Alisema kuuwa mikataba ya kibiashara pekee haitoshi kufanikisha mtangamano wa kiuchumi bila kuwa na mifumo jumuishi ya usafirishaji inayounganisha bandari, barabara, reli, vituo vya mizigo, maeneo ya viwanda na masoko.


