Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
SHIRIKA la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limesema asilimia 50 ya mkaa mbadala unaotumia katika maeneo mbalimbali hauna ubora kutokana na watengenezaji wake kufanya shughuli hiyo bila kupata mafunzo yakitaalamu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO Profesa Mkumbukwa Mtambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 7,amesema takwimu hiyo imetokana na tafiti waliyofanya katika mikoa 12 kwa ajili ya kuwabaini wanaotumia mkaa mbadala kupitia mradi wa kukuza matumizi wa nishati hiyo ambapo mkoa wa Dar es Salaam umeonekana kuongoza kuwa na watumiaji wengi.
“Mradi huu ulianza mwaka 2022,lakini katika kufanya utafiti tulianza kuwabaini watengenezaji wa mkaa mbadala katika mikoa 12 ambapo tulikusanya takribani watumiaji 59,katika kuangalia ubora wa mkaa tulikuta sampuli zaidi ya 43 ambazo ni zaidi asilimia 50 hazina ubora,”amesema Profesa Mtambo.
Amesema kupitia utafiti huo pia wamegundua changamoto za malighafi ya utengenezaji wa mkaa mbadala ambapo imeonekana watengenezaji wengi wanatumia mabaki ya mkaa yanayotokana na kuni ambayo yanatoa mkaa wenye ubora ambao wanaupiga vita.
“Kutokana na hali hiyo tumetoa mafunzo kwa watengenezaji zaidi ya 30 kwenye mikoa 11 tuliyoifanyia utafiti na tunaendelea kuwaita watengenezaji wengine waje kupata mafunzo Tirdo,”amesema Profesa Mtambo.
Amesema mbali na hilo utafiti pia umeonyesha wanaopaswa kutumia mkaa mbadala hasa taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 ambazo ni 127 zilizofanyiwa utafiti asilimia 52 bado wanatumia kuni hivyo changamoto bado ipo.
Profesa Mtambo amewakaribisha watengenezaji wa mkaa na watumiaji kufika katika ofisi hiyo kwa ajili ya utengenezaji wa nishati hiyo kupitia mradi hio ambao unaendelea.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA) Dk.Donald Mmari amesema wameshriki katika mradi huku akisema moja ya jambo ambalo wamelibaini katika tafiti ni uharibifi wa mazingora unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni nchini.
“Mwaka 2015 upotevu wa misitu hekta 372,000 lakini maiaka saba bada yaani ilipofika mwaka 2022 upotevu umefika hekta takribani 400,000 tukaona hiyo ni mbaya sana,watu wanakata miti inaleta madhara ikiwemo hewa ya ukaa lakini pia kuongezeka kwa ukame na majanga,”amesema Dk.Mmari.
Amesema kama taasisi waliona wafanye utafiti ambapo walianza kwakuangalia kuhusu utumiaji wa mkaa na faida zake kiafya.