Na Mwandishi Wetu,Manyara
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mnada wa madini ya vito unaotarajiwa kufanyika katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ili kuyaongezea thamani madini hayo.
Mnada huo ambao ulisimama kwa muda, umepangwa kufanyika tena kwa mara ya kwanza Desemba 14, 2024.
Akizungumza leo Desemba 12,2024 Mavunde amesema madini ya vito, yanafanyiwa mnada kama mkakati wa kuyatangaza na kuyaongezea thamani kimataifa.
Mavunde amesema utaratibu wa kufanya mnada huo ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi na pia kuwasaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na soko la dunia.
Amesema, mnada huo utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi na atakayenunua madini hayo katika mnada ni atakayeshinda bei iliyowekwa.
“Mnada huu utaendeshwa kwa usalama mkubwa kwa kuwa madini hayo hususan Tanzanite yana thamani kubwa. Serikali imeimarisha ulinzi ili kujihadhari na watu wasio waaminifu,”amesema Waziri Mavunde.
Aidha, amesema mnada huo utaiwezesha Serikali kupata mrabaha stahiki na kodi kwa uwazi ili kuchangia pato la Taifa na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wauzaji, wanunuzi na mali zao.
Minada kama hiyo pia hufanyika kwa nchi za Afrika zenye madini ya vito kama vile Zambia (emerald), Zimbabwe (almasi) na Afrika Kusini (almasi).