Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
ZAIDI ya wafanyabiashara 3,752 waliopo nchini pamoja na nchi 23 zinatarajiwa kushiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) yatayoanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 24, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade Dk.Ratifa Mohamed Khamisi alisema maonesho ya yanatarajiwa kuanza Juni 28 na kumalizika Julai 13 mwaka huu ambapo wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi watapata fursa yakutangaza biashara zao kupitia jukwaa hilo ambalo lipo kimataifa zaidi.

“Mpaka sasa jumla ya kampuni 3752 zimejiandikisha kushiriki ambapo idadi imeongezeka tofauti na mwaka jana ambayo ilikuwa 3670 ,pia tunatarajia kupata washiriki kutoka 23 na tumeshaanza kuwapokea na tunatarajia kuwapokea zaidi,”alisema Dk.Ratifa.
Alisema maonesho ya mwaka huu yataenda sambamba na shamrashamra za sherehe ya Jubilee ya Dhahabu ya kutimiza miaka 50 ya taasisi hiyo ambapo kwakuanza Juni 26 kutakuwa na semina ya washiriki wa maonesho hayo kwa lengo la kuelekezana mambo mbali mbali yanayohusu maonesho.
“Maonesho ya miaka hii 50 pia yataambatana na sherehe ya Jubilee ya Dhahabu,Juni 26 tunafanya semina ya washiriki wote,semina hii inaleta tija ya maonesho ni muhimu kwa sababu kuna wageni wenyeji,tunaelekezana utaratibu na sheria za maonesho,ukipata tatizo gani ufanye nini,”alisema Dk.Ratifa.

Alisema mbali na semina pia kutakuwa na matembezi yatakayofanyika Juni 27 asubuhi ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania Mussa Azzan Zungu akisindikizwa na viongozi wa wizara viwanda na biashara,viongozi wa Tantrade pamoja wananchi wa Temeke ambapo matembezi yataanzia katika uwanja wa Farasi mpaka katika ofisi za Tantrade.
“Hatutaishia hapo tu kwakuwa hizi ni sherehe kubwa za kutimiza miaka 50 usiku wa kuamika Juni 27 pia tutapiga fashi fashi na fataki kuonesha ishara ya kuelekea miaka 50,”alisema Dk.Ratifa.
Alisema pia kutakuwa na usiku maalum wa Golden Jubilee ambapo utafanyika Julai sita utakaombatana na kutoa tuzo na kwa washindi wa mabanda pamoja na kuwatambua watu mbalimbali wanaoleta tija kwenye maonesho,wadau wanaochangia kufanikisha mapnesho hayo pamoja na washiriki wanaoshiriki kila mwaka.
Alisema katika maonesho ya mwaka huu kauli mbiyu ni
‘Maonesho ya Kimataifa ya Sabababa ni fahari ya Tanzania’ pamoja na kauli mbiyu ndogo inayosema bidhaa za Tanzania Kitaifa zaidi,biashara za Tanzania Kidigitali zaidi huku neno la hamasa ni ‘sabasba 2026 hii ni kubwa kuliko’.


