๐Lengo ni kukidhi matarajio ya wananchi katika Sekta ya Nishati
Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka watendaji na watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao katika mwaka mpya wa fedha 2026/2027 ili kuweza kukidhi matarajio makubwa ya wananchi katika sekta ya nishati.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo katika kikao kazi kilichojumuisha viongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kilicholenga kupata matokeo ya tathmini ya utendaji kazi wa Wizara na taasisi hizo.

Kikao kazi hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba na Makatibu Wakuu, Mhandisi Felchesmi Mramba na Dkt.James Mataragio.
Waziri Ndejembi amesema wananchi wanamatarajio mbalimbali ikiwemo kupata umeme wa uhakika, kuongezeka kwa uzalishaji na matumizi ya gesi asilia na mafuta, uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini pamoja na nishati safi ya kupikia.

“Mwaka wa fedha unaokuja twendeni tukachape kazi, Watanzania wanamatarajio makubwa sana. Wana matarajio ya kuwa na umeme wa uhakika, wana matarajio ya kuona gesi ikiongeza uzalishaji, wana matarajio ya kuona vitalu vyetu vinapata wawekezaji, na vile ambavyo vina wawekezaji basi wanachimba. Wana matarajio ya kuona kwamba mafuta hayaishi ndani ya Tanzania.” Amesema Mhe. Ndejembi
Aidha, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana imani kubwa na Wizara ya Nishati, jambo linalodhihirishwa na kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ya nishati nchini.


