Na Mwandisbi Wetu, Uingereza
Serikali ya Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu ya usafirishaji wa umeme ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza katika kikao cha pembeni ya Wiki ya Mazingira ya London (London Climate Week) kilichoandaliwa na Serikali za Uingereza na Brazil pamoja na Benki ya Dunia, chini ya mpango wa Global Clean Power Alliance (GCPA) Finance Mission Machi 24,2026 jijini London, Uingereza, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila, amesema mahitaji ya umeme nchini yanaongezeka kwa wastani wa asilimia 10 hadi 15 kila mwaka.

Amesema Serikali inalenga kuongeza takribani megawati 3,700 za uwezo wa uzalishaji wa umeme ifikapo mwaka 2030 ili kusaidia maendeleo ya viwanda, mageuzi ya kiuchumi na upatikanaji wa umeme kwa wananchi wote.
Mhandisi Rwebangila amesema kuwa kutokana na changamoto za upatikanaji wa fedha za umma, Serikali imeweka mazingira bora yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa miradi ya umeme.
Ameongeza kuwa Kupitia Mpango wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact), Tanzania inalenga kuvutia zaidi ya dola bilioni nne za Marekani kutoka kwa wawekezaji binafsi ifikapo mwaka 2030 ili kusaidia utekelezaji wa malengo ya sekta ya nishati.

Aidha, amesema Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2020, sambamba na uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa mwaka 2023 kuruhusu ushiriki wa sekta binafsi katika usafirishaji wa umeme, umefungua fursa mpya za uwekezaji katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa TANESCO tayari imepokea maombi na maelezo ya awali kutoka kwa wawekezaji mbalimbali, jambo linaloashiria kuongezeka kwa hamasa ya kuwekeza katika miradi ya usafirishaji wa umeme nchini.
Hata hivyo, amesema bado kuna haja ya kuimarisha maandalizi ya miradi, mifumo ya mgawanyo wa vihatarishi (risks allocation) kati ya Serikali na Sekta Binafsi, mikataba na nyaraka za zabuni ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na mvuto kwa wawekezaji huku ikiendelea kuwa nafuu kwa wananchi.

Mhandisi Rwebangila amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo katika kuandaa miradi yenye tija, akieleza kuwa miundombinu imara ya usafirishaji wa umeme ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda, ajira na ustawi wa wananchi.


