Na Mwandishi Wetu,Arusha
KAMPUNI ya Kitanzania ya Ngoteya Wild, inayoongozwa na muandaaji wa makala zenye maudhui ya uhifadhi na wanyamapori @Hans_Cosmas_Ngoteya, imetangaza kuwa filamu yao mpya ya Sentinels of Engaruka ambayo wamefanya kwa kushirikiana na African people and wildlife itaoneshwa rasmi kupitia YouTube channel yao tarehe 21 Juni 2026.
Filamu hiyo imechukua zaidi ya miaka mitatu kuandaliwa, ikihusisha utafiti wa kina, upigaji picha wa mazingira ya asili na simulizi inayoonesha uhusiano wa kipekee kati ya jamii ya Kimasai, twiga na mazingira ya Engaruka mkoani Arusha. Toleo la Kiswahili la filamu hiyo limesimuliwa na mtangazaji maarufu Meena Ally, ambaye sauti yake itaongeza mguso wa kipekee katika kuifikisha hadithi hiyo kwa watazamaji wa Tanzania na Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Hans Ngoteya, filamu hiyo inalenga kuhamasisha uhifadhi wa maliasili, kuonesha utajiri wa urithi wa Tanzania na kuifikisha hadithi ya Engaruka kwa hadhira ya kimataifa kupitia jukwaa la YouTube.
Sentinels of Engaruka ni moja ya miradi mikubwa ya filamu za uhifadhi iliyotayarishwa nchini Tanzania, ikiwa na lengo la kuonesha namna jamii na wanyamapori wanavyoweza kuishi kwa maelewano huku wakilinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Usipange kukosa kutazama filamu hii 21.06.2026 katika ukurasa wa youtube wa @Ngoteyawild .


