TANZANIA ,ANGOLA ZATAKIWA KUONGEZA BIASHARA,TISEZA YANADI FURSA YANADI FURSA ZA UWEKEZAJI

Na Mwandishi Wetu

Tanzania, Angola zatakiwa kuongeza biashara, TISEZA yanadi fursa za uwekezaji

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Tanzania na Angola zimetakiwa kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili kwa kutumia fursa zilizopo katika sekta za viwanda, kilimo, nishati na usafirishaji ili kugeuza uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia kuwa manufaa ya kiuchumi.

Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Angola yaliyofanyika katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, ambapo Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilinadi fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Said Seif Mzee, alisema Tanzania na Angola zina historia ndefu ya ushirikiano wa kisiasa tangu enzi za harakati za ukombozi, lakini sasa kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

“Leo tumefanya maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Angola katika Maonesho ya Sabasaba. Tumebadilishana taarifa kuhusu fursa zilizopo katika nchi zetu, hivyo ni wakati sasa wafanyabiashara na wawekezaji kuchangamkia fursa hizo ili kuongeza biashara na uwekezaji,” alisema.

Alisema kiwango cha biashara kati ya nchi hizo bado hakijafikia matarajio, huku Tanzania ikiendelea kusafirisha bidhaa nyingi zaidi kwenda Angola kuliko zinazoingizwa kutoka nchi hiyo.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuwahamasisha wawekezaji wa Angola kuwekeza nchini katika sekta za viwanda, biashara na kilimo kutokana na mazingira bora ya uwekezaji yaliyopo.

Kwa upande wake, Balozi wa Angola nchini Tanzania, Domingos De Almeida Da Silva Coelho, alisema wakati umefika kwa Tanzania na Angola kugeuza urafiki wa kihistoria kuwa ushirikiano wa kibiashara wenye matokeo chanya kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

“Angola na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu wa kirafiki, lakini sasa tunahitaji kuona ushirikiano huo ukizalisha ajira, kuongeza biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema.

Naye Ofisa Mwandamizi wa Uwekezaji wa TISEZA, Vedasto Kagombora, alisema mamlaka hiyo imeendelea kunadi maeneo maalum ya kiuchumi na maeneo ya uzalishaji kwa ajili ya mauzo nje ya nchi ili kuvutia wawekezaji kutoka Angola na mataifa mengine.

Alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia mageuzi ya sera na mifumo ya udhibiti ili kuongeza ushindani na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji katika Afrika Mashariki.

“Tunaendelea kuboresha huduma kwa wawekezaji kwa kupunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa eneo lenye mazingira rafiki ya kufanya biashara,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Afritrack, Sebena Yohannes, alisema Maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wafanyabiashara, wawekezaji na wazalishaji kutoka mataifa mbalimbali, hatua inayochochea biashara na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.

Washiriki wa mkutano huo walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta za kilimo, viwanda, nishati na usafirishaji, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza biashara na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi kwa nchi za Afrika.