Na Aziza Masoud, Dodoma
CHAMA Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMKU LTD) kimeeleza mpango wa kujenga kiwanda cha kuchakata korosho wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ili kuongeza thamani ya zao hilo, kuboresha soko na kuinua kipato cha wakulima.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijink Dodoma, Mjumbe wa Bodi ya TAMKU, Nurudini Rajabu Chikolo, alisema mradi huo ni sehemu ya dira ya maendeleo ya chama hadi mwaka 2050 na unalenga kuifanya Tunduru kuwa kitovu cha uchakataji wa korosho.

Alisema pamoja na kiwanda hicho, TAMKU pia imepanga kujenga jengo la utawala la ghorofa tano litakalogharimu takribani Sh bilioni saba, likiwa na ukumbi wa kisasa wenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 700.
“Maandalizi ya awali ya ujenzi tayari yameanza, ikiwemo kukamilisha taratibu za vibali na michoro ya uhandisi. Ujenzi utaanza mara taratibu hizo zitakapokamilika,” alisema Chikolo.

Alisema uwekezaji huo unakuja baada ya chama kuimarisha shughuli zake za ushirika kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na huduma za usafirishaji wa mazao, hatua zilizosaidia kuongeza ufanisi katika mnyororo wa thamani wa mazao.
Alisema kwa sasa, TAMKU inamiliki malori matano yanayotoa huduma za usafirishaji wa mizigo nchini kote, huku kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ikihudumia mazao ya korosho, ufuta na mbaazi katika Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma na maeneo jirani, ikiwemo Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Aliongeza kuwa kampuni tanzu ya TAMKU Group of Companies Limited inasimamia maghala ya kuhifadhi mazao, kupokea mazao ya wakulima na kusambaza pembejeo za ruzuku, hatua zinazochangia kuongeza uzalishaji na mapato ya wanachama.

Chikolo alisema mafanikio hayo yameiwezesha TAMKU kupanga uwekezaji mkubwa zaidi, huku uzalishaji wa korosho ukiongezeka kutoka tani 17 mwaka 2017 hadi tani 41,000 katika msimu uliopita.
Aidha, aliwahimiza vijana kujiunga na vyama vya ushirika ili kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo, akisisitiza kuwa ushirika una nafasi muhimu katika kuongeza ajira, ubunifu na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima, akisema hatua hiyo imechangia kuongezeka kwa uzalishaji na kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kiwanda hicho cha korosho.


