NISHATI NI CHACHU YA KILIMO, UCHUMI NA MAENDELEO YA VIJIJINI – MHA. SAIDY
Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy, amewakaribisha wananchi na wadau kutoka sekta mbalimbali kutembelea Banda la REA katika Maonesho ya Nane Nane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ili kujionea mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini na kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala.
Akizungumza kuhusu maonesho hayo, Mha. Saidy amesema REA inaendelea kutekeleza miradi ya umeme vijijini na nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati zote kwa wananchi ili kuchochea shughuli za uzalishaji, kuboresha huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Ameeleza kuwa upatikanaji wa nishati bora umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwezesha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, ikiwemo umwagiliaji, uchakataji na uhifadhi wa mazao, pamoja na kukuza biashara na viwanda vidogo vijijini. Hali hiyo imechangia kuongeza tija, kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mha. Saidy amesisitiza kuwa Banda la REA ni fursa muhimu kwa wananchi na wadau kupata elimu kuhusu utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini, kufahamu mafanikio yaliyopatikana na kuelewa mchango wa nishati katika kuimarisha maendeleo ya wananchi hususan waishio vijijini ili kuitekeleza kivitendo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


