TUZO SHINDANI KUONGEZA TIJA YA SEKTA YA MAZIWA


Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Wafugaji nchini wanatarajiwa kuongeza tija na uzalishaji wa maziwa kupitia mradi wa Tuzo kwa Tasnia ya Maziwa Himilivu kwa Tabianchi, linalolenga kuhamasisha sekta binafsi kuongeza upatikanaji wa pembejeo na huduma bora za mifugo.


Mradi huu wa miaka miwili umeanza mwaka 2026 hadi 2028, na unatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Morogoro. Mradi unalenga kuongeza uzalishaji wa maziwa, kipato cha wafugaji na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.


Mradi huu upo chini ya AgResults, ambayo imeandaa mfumo wa Malipo kwa Matokeo na kusimamia muundo wa tuzo. Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, itaendelea kutoa miongozo ya kisera na kisekta pamoja na kuhakikisha utekelezaji wake unaendana na vipaumbele vya taifa, huku Heifer International ikiwa Msimamizi wa Mradi anayesimamia utekelezaji na uratibu wa wadau nchini.


Akizindua mradi huo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, alisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kuongeza tija katika sekta ya maziwa kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia, malisho bora na huduma bora za mifugo.


“Mafanikio hayapaswi kupimwa kwa fedha za tuzo zitakazotolewa, bali kwa mabadiliko yatakayoletwa katika ngazi ya mfugaji na soko, hususan pale wafugaji wadogo, wanawake na vijana watakapopata huduma bora na fursa za kukuza biashara zao,” alisema Kamani.


Alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu mbegu na malisho bora, afya ya mifugo, uhimilishaji na teknolojia zinazoweza kuongeza uzalishaji.


Kamani alisema changamoto ya uzalishaji mdogo wa maziwa inahitaji ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wafugaji na washirika wa maendeleo ili kuongeza tija, kuimarisha masoko na kuboresha kipato cha wafugaji.


Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Profesa George Msalya, alisema shindano hilo litachangia kuongeza uzalishaji na masoko ya maziwa, sambamba na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wafugaji.
Alisema upatikanaji wa pembejeo na huduma bora utawasaidia wafugaji kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kujenga uhusiano wa kudumu na masoko rasmi.


Mkurugenzi wa Heifer International nchini Tanzania, Mark Tsoxo, alisema sekta ya maziwa ni chanzo muhimu cha chakula, ajira na kipato, lakini bado inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya ya mifugo, uhimilishaji, ushauri wa kitaalamu na malisho bora.


Alisema Heifer International, katika nafasi yake kama Msimamizi wa Mradi, itaratibu utekelezaji wa shindano na kufanya kazi na Serikali, AgResults, sekta binafsi na wadau wengine kuhakikisha huduma zinawafikia wafugaji wanaolengwa.


“Kupitia motisha zinazotegemea utendaji, shindano hili litachochea ubunifu wa sekta binafsi na kupanua upatikanaji wa huduma bora kwa wafugaji wadogo,” alisema Tsoxo.


Mwakilishi wa Sekretarieti ya AgResults, Markus Mueller, alisema shindano hilo ni sehemu ya uzoefu wa zaidi ya miaka 10 wa AgResults katika kutumia mfumo wa Malipo kwa Matokeo kukabiliana na changamoto za maendeleo ya kilimo.


“Wafanyabiashara wanapotuzwa kwa matokeo yaliyothibitishwa badala ya shughuli pekee, hubuni njia mpya za kuwafikia wafugaji, kuondoa vikwazo vya masoko na kujenga uhusiano wa kudumu wa kibiashara. Tunatarajia kuona ubunifu na ushirikiano utakaoibuka kupitia shindano hili nchini Tanzania,” alisema Mueller.


Kiongozi wa Mradi kutoka Heifer International, Elina Lusuva, alisema shindano litawahamasisha watoa huduma kuongeza upatikanaji wa chanjo, huduma za kudhibiti vimelea, uhimilishaji, ushauri wa kitaalamu na malisho yaliyoboreshwa.


Alisema mradi unatarajiwa kuwafikia takribani wafugaji wadogo wa maziwa wapatao 28,200 na kuchangia uzalishaji wa tani 7,500 za ziada za malisho yaliyoboreshwa.


Mradi huo unashirikiana na Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa Himilivu kwa Tabianchi, ambao ni uwekezaji wa miaka 10 wenye thamani ya dola milioni 231 wa Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo. Ushirikiano huo unasaidia Serikali kutekeleza vipaumbele vyake vya kuongeza tija, kuimarisha masoko na kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi katika mnyororo wa thamani wa maziwa.


Aidha, Mradi ni sehemu ya AgResults, mpango shirikishi unaoungwa mkono na serikali za Australia, Canada, Uingereza na Marekani, pamoja na Gates Foundation na World Bank.


Kwa upande wao, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na CRDB Bank zilieleza kuwa wafugaji na watoa huduma watapata fursa za huduma za kifedha na mitaji ya kuendeleza shughuli zao, huku wakihimizwa kuwekeza katika uzalishaji wenye tija.


Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Maziwa, Hamisi Mzee, alisema wafugaji wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Serikali na wadau na watahakikisha wanayafanyia kazi ili kuongeza uzalishaji.


Naye Anna Almas, mzalishaji wa maziwa kutoka Mvomero, alisema wadau wanapaswa kutumia fursa inayotolewa na mradi huu kuboresha uzalishaji, malisho na huduma kwa wafugaji ili kuifanya sekta ya maziwa kuwa na tija na ushindani zaidi.
Mwisho