Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WANAHABARI na watengeneza maudhui kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kuitangaza Tanzania kwa hadhira ya kimataifa kupitia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), huku vivutio vya utalii, utamaduni na maandalizi ya michuano hiyo vikitajwa kuwa sehemu ya maudhui yatakayosambazwa nje ya nchi.
Wanahabari hao kutoka Marekani, Canada, Afrika Kusini, Ufaransa na Uingereza wamealikwa nchini kupitia kampeni ya Destination Tanzania, inayolenga kutumia nguvu ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbas, amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kuwapokea wanahabari na watengeneza maudhui hao, walioanza ziara ya siku saba nchini.
Amesema ziara hiyo inalenga kuwapa fursa ya kuifahamu Tanzania kwa karibu, kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kushuhudia maandalizi ya nchi kuelekea AFCON, ili baadaye kutumia majukwaa yao kufikisha taarifa hizo kwa hadhira kubwa nje ya Tanzania.

“Kupitia ziara hii, Tanzania inalenga kutumia ushawishi wa wanahabari na watengeneza maudhui hawa kufikisha ujumbe kuhusu utalii, michezo, utamaduni na fursa nyingine zilizopo nchini kwa hadhira kubwa nje ya Tanzania,” amesema Dk. Abbas.
Amesema kupitia uzoefu watakaoupata nchini, wanahabari hao watakuwa na nafasi ya kueleza kwa hadhira zao mambo wanayoyaona na kuyashuhudia moja kwa moja, ikiwamo vivutio vya utalii na maandalizi ya Tanzania kuelekea michuano hiyo.

Dk. Abbas amewaalika wanahabari hao kurejea nchini wakati wa AFCON ili kushuhudia na kuripoti michuano hiyo pamoja na uzoefu wa Tanzania kama mwenyeji.
Kwa upande wake, John Jackson, Mtanzania aliyehusika kuwaalika wageni hao nchini, amesema ziara hiyo inalenga kuwapa uzoefu wa moja kwa moja kuhusu Tanzania ambao utawasaidia kutengeneza maudhui yanayoweza kuwafikia watu wengi katika mataifa yao.

Amesema katika kipindi cha siku saba, wageni hao watatembelea maeneo mbalimbali ya utalii, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar, huku wakipata pia fursa ya kuona miundombinu ya michezo.
“Wageni hawa katika kipindi cha siku saba watatembelea maeneo mbalimbali ya utalii, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar, huku pia wakipata fursa ya kuona miundombinu ya michezo,” amesema Jackson.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dk. Theresa Mugobi, amesema kampeni ya Destination Tanzania inalenga kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu vivutio na fursa mbalimbali za utalii zilizopo nchini.
Amesema ushiriki wa wanahabari na watengeneza maudhui kutoka mataifa hayo utasaidia kufikisha ujumbe kuhusu Tanzania katika masoko mbalimbali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Wanahabari na watengeneza maudhui walioshiriki ziara hiyo ni Sara Poraria kutoka Canada, Karina Bermudez kutoka Marekani, Geneefah Lee kutoka Afrika Kusini, Alizee Morat kutoka Ufaransa, pamoja na Adam Britton na Cameroon James kutoka Uingereza.


