PROF GURUMO AITANGAZA TANZANIA KIMATAIFA KUPITIA SEKTA YA BAHARI

Na Mwandishi Wetu

Mchango wa Watanzania katika kuendeleza sekta ya bahari kimataifa umezidi kutambuliwa baada ya Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Prof Tumaini Shabani Gurumo kutunukiwa tuzo ya heshima ya Mwanafunzi wa Zamani Mashuhuri (Outstanding Alumna Award) kutoka Chuo Kikuu cha World Maritime University (WMU) kilichopo nchini Sweden.

Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha uongozi, elimu na mafunzo ya sekta ya bahari pamoja na kuchochea maendeleo ya taasisi zinazohusika na sekta hiyo barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani Bwana Arsenio Dominguez alimkabishi Prof Gurumo tuzo hiyo Oktoba 31 Mwaka huu katika mahafali ya 43 ya (WMU) yaliyofanyika nchini Sweden mbele ya Mgeni Rasmi ,Mwenyekiti wa Bodi Tendaji ya chuo hicho na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Jiji la Malmo.

Aidha Prof Gurumo amekuwa na mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya bahari hususani katika uongozi, utafiti katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa sekta hiyo.

Prof Gurumo Amefanya kazi katika sekta ya bahari kwa zaidi ya miaka 20 ambapo miaka 10 ameitumikia katika nafasi mbalimbali za usimamizi na uongozi Katika kipindi hicho huku akijihusisha na ufundishaji wa sheria za bahari kwa wataalamu wenye uzoefu na wanaoanza taaluma katika maeneo ya bandari, usafirishaji wa majini na masuala ya bahari.

Akizungumzia mchango wake Rais wa (WMU) Profesa Maximo Mejia Jr amesema kuwa Prof Gurumo ametumia sehemu kubwa ya maisha yake ya kitaaluma kuendeleza sekta ya bahari kupitia ufundishaji, utafiti na ushauri wa kitaalamu.

Hata hivyo Prof Gurumo ni mtafiti na mwandishi wa machapisho mbalimbali ikiwemo kitabu kinachohusu Uchumi wa Buluu, Fursa, na Chachu ya Maendeleo huku akifanya kazi kama mshauri wa kitaalamu katika masuala ya uchumi wa buluu na usafirishaji wa majini kwa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) na TradeMark East Africa (TMEA).

“Kupitia Mchango wake ameboresha elimu na mafunzo ya sekta ya bahari ikiwa ni hatua iliyosaidia kuimarisha viwango vya ubora na kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi wa kutekeleza majukumu yao katika meli, bandari, na mamlaka za usimamizi wa bahari na usafirishaji wa mizigo.” Amesema Prof Mejia Jr.”

Katika hatua nyingine Prof Gurumo alihitimu Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Kampasi ya Iringa mwaka 2004, kabla ya kupata Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Masuala ya Bahari na kubobea Sheria na Sera kutoka (WMU) mwaka 2007 Mwaka 2012 alipata Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kimataifa za Bahari kutoka Dalian Maritime University nchini China.

Katika mahafali hayo Watanzania wengine wanne walitunukiwa vyeti vya kuhitimu shahada ya uzamili na stashahada katika fani mbalimbali za sekta ya bahari.

Mafanikio hayo yanatarajiwa kuongeza nguvu katika upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi wa kimataifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika maendeleo ya sekta ya bahari na uchumi wa buluu barani Afrika.