Na Mwandishi Wetu,Morogoro
VIONGOZI kutoka Wizara tano mtambuka wamekutana mkoani Morogoro kujadili njia za pamoja katika utekelezaji wa mradi wa bwawa la Maji Kidunda ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Akiongoza kikao kazi hicho Katibu Mkuu Wizara ya maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amesisitiza ushirikiano wa ki sekta katika utekelezaji wa mradi wa bwawa la Kidunda unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

“Tumekutana Wizara muhimu za kisekta zinazochangia ukamilishaji wa Mradi wa Kidunda ili kubaini maendeleo ya mradi sambamba na kukwamua changamoto zilizopo ili mradi ukamilike kwa wakati, ushirikiano wa kisekta ni muhimu sana kwani kwa pamoja tutasaidiana kutatua changamoto na kuja na mipango bora zaidi ya utekelezaji wa mradi huu muhimu kwa wananchi” ameeleza Mhandisi Mwajuma.
Mhandisi Mwajuma ameongeza kuwa katika kipindi cha utekelezaji wa mradi ni muhimu kushirikiana kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira na ulinzi wa vyanzo vya maji ili pindi bwawa litakapokamilika kusiwepo na changamoto za uharibifu wa mazingira na kupelekea bwawa kutojaa inavyohitajika.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt Musa Ali Musa ametoa maelezo kwa watekelezaji wa mradi wa bwawa la Kidunda kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wananchi wanaozunguka mradi huu ili kuepuka malalamiko yanayoweza kuleta dosari katika mradi.
Wizara zilizokutana ni Wizara ya Maji, Wizara ya Mifugo na Uvivu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Tume ya .. na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 329 utanufaisha mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani na Morogoro katika huduma za upatikanaji majisafi.


