Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WANANCHI wengi nchini wameendelea kujitokeza kuwasilisha kero zao moja kwa moja serikalini kupitia mifumo ya kisasa ya mawasiliano, huku migogoro ya ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia vikitajwa kuongoza kwa wingi wa malalamiko.
Hatua hiyo imechochea jitihada za serikali kuimarisha upatikanaji wa haki kwa haraka kupitia majukwaa ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera, amesema kupitia kituo cha huduma kwa wateja pamoja na programu ya “Sema na Waziri” inayofanyika mara tatu kwa mwezi, wamekuwa wakipokea na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

“Kwenye kituo hiki cha huduma kwa wateja, changamoto kubwa zinazowasilishwa na wananchi ni mirathi, ndoa za utotoni na zaidi migogoro ya ardhi,” alisema Dk. Homera.
Alifafanua kuwa serikali imeweka utaratibu wa kushirikiana kati ya wizara mbalimbali ili kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati, akitolea mfano Wizara ya Ardhi ambayo imekuwa mstari wa mbele kushughulikia migogoro hiyo.
Aidha, alisema wizara yake ina wataalamu wa sheria, wakiwemo mawakili na washauri wa kisheria, pamoja na kushirikiana na mihimili mingine ya utoaji haki ikiwemo mahakama, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwananchi.

Alieleza kuwa wanapokea changamoto kwa njia mbalimbali ikiwemo WhatsApp, barua pepe, simu na ana kwa ana, huku baadhi ya kesi zikiwasilishwa kwa maandishi na wahusika kuitwa wizarani kwa ajili ya usuluhishi.
“Wananchi wakifika wizarani, tunapobaini changamoto zao zinahusu wizara nyingine, tunawasiliana nazo mara moja. Hakuna jambo linalofikishwa serikalini likakosa suluhu, kwa sababu serikali ina majibu na haki itatendeka,” alisisitiza.
Dk.Homera alisema dhamira ya serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati, na kwamba wizara hiyo inaendelea kusaidia kwa kiwango kikubwa kufikia azma hiyo.

Aliongeza kuwa Aprili 22 mwaka huu watatoa mrejesho kwa wananchi wote waliowasilisha changamoto zao, pamoja na kuendelea kupokea simu na ujumbe mpya ili kuhakikisha matatizo yanatatuliwa kwa wakati.
Akizungumzia ukatili wa kijinsia, alisema bado wanawake wengi wanaofanyiwa ukatili wanashindwa kutoa taarifa kwa kuhofia kuvunja ndoa zao, hali inayoweza kuhatarisha maisha yao.
Aliwataka wananchi wanaokumbana na vitendo vya ukatili kutoa taarifa katika ngazi za serikali za mitaa ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa haraka.

Kwa mujibu wa waziri huyo, hadi sasa wamepokea zaidi ya simu 20 kwa siku, huku nyingi zikihusu migogoro ya ardhi, unyanyasaji wa kijinsia, mirathi na masuala ya ndoa.
Alisema pia wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha wa haki zao na njia sahihi za kutafuta suluhu ya changamoto zao.
Akitoa takwimu, Dk. Homera alisema tangu kuanzishwa kwa programu ya “Sema na Waziri”, jumla ya simu 2,236 zimepokelewa, ambapo asilimia 69 ya malalamiko hayo tayari yameshafanyiwa kazi, huku asilimia 31 yakiendelea kushughulikiwa.


