SERIKALI YAJIPANGA UPYA SEKTA YA MADINI, YAFUTA LESENI 40 ZISIZOENDELEZWA

Na Asha Mwakyonde,DODOMA

SERIKALI kupitia Tume ya Madini imechukua hatua ya kufuta jumla ya leseni 40 za utafutaji wa madini kutokana na wamiliki wake kushindwa kuziendeleza, katika juhudi za kuimarisha usimamizi wa rasilimali za madini nchini na kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania kwa tija.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 15, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema leseni hizo zimefutwa baada ya wamiliki wake kushindwa kutekeleza masharti ya uendelezaji licha ya kupewa hati za makosa na muda wa kurekebisha kasoro zilizobainishwa.

Amesema leseni hizo zitarudishwa Serikalini na zitapangiwa utaratibu mpya wa kugawiwa kwa wachimbaji wadogo, wawekezaji wenye nia na uwezo wa kuendeleza miradi, pamoja na makundi ya wanawake na vijana kupitia programu ya Mining for A Brighter Tomorrow (MBT).

“Wapo waliokuwa wanamiliki leseni lakini hawafanyi uwekezaji wowote unaoonekana, wala kuthibitisha matumizi ya fedha katika kuendeleza maeneo yao. Hali hii hairuhusiwi kuendelea,” amesema Mavunde.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, tathmini ya kina iliyofanywa na Wizara ya Madini imebaini ukiukwaji mkubwa wa masharti ya leseni, ikiwemo kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, kushindwa kulipa ada stahiki, kutotekeleza wajibu wa ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content) pamoja na kushindwa kutekeleza miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).

“Hizi leseni 40 ni sawa na eneo lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba 900, sawa na hekta 188,163,” amefafanua.

Aidha, Serikali kupitia Tume ya Madini imetoa hati za makosa kwa leseni nyingine 43, zikiwemo leseni 40 za utafutaji na tatu za uchimbaji wa kati, ambapo wamiliki wake wametakiwa kurekebisha kasoro ndani ya siku 30.

Akizungumzia ongezeko la matukio ya uvamizi katika maeneo yenye madini maarufu kama “gold rush”, Mhe. Mavunde ametoa onyo kali kwa watu wanaoingia katika maeneo yenye leseni halali bila kufuata sheria, akisisitiza kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa.

“Uchimbaji wowote bila leseni ni kinyume cha sheria na hautavumiliwa,” amesema, akibainisha kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha migogoro, uharibifu wa mazingira na hatari za kiafya.

Amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwemo kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao, kuzuia migogoro ya umiliki, kulinda mazingira dhidi ya uchimbaji holela na kudhibiti milipuko ya magonjwa katika maeneo yenye msongamano wa wachimbaji.

Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia maeneo yenye leseni halali, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka sheria.

“Kuanzia sasa ni marufuku kuvamia maeneo ya leseni kwa sababu yoyote ile. Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wote watakaohusika,” amesisitiza.