Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na taasisi nyingine za mafunzo ya ufundi kutumia fursa za maonesho kama jukwaa la kujitangaza na kuonesha ubunifu,ujuzi na teknolojia ili kuongeza thamani ya bidhaa.
Kaulo hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda Balozi Waziri Salum alipotembelea banda la VETA katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yaliyoanza Juni 28 katika viwanja vya Mwalimu Nyerere maarufu kama Sabasaba.

Alisema maonesho yoyote yanayofanyika ndani na nje ya nchi yanatakiwa kutumika kama jukwaa la kuonesha ubunifu, ujuzi na teknolojia zinazozalisha ajira na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania.
Balozi Salum alisema maandalizi yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 99 na kwamba Serikali inatarajia maonesho ya mwaka huu kuwa miongoni mwa yenye mafanikio makubwa.

Alisisitiza kuwa taasisi za mafunzo kama VETA zina nafasi muhimu ya kuandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda.
“Maonesho hayo yanapaswa kutumiwa si kwa ajili ya kuuza bidhaa pekee, bali pia kujenga ushirikiano wa kibiashara, kutafuta masoko mapya na kuonesha uwezo wa Watanzania katika ubunifu na uzalishaji wa bidhaa zenye viwango vya kimataifa,”alisema Balozi Salum.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alieleza kuridhishwa na ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini, hususan zile zinazotengenezwa na wajasiriamali wanawake, akisema zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa katika ubora na vifungashio na sasa zinaweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wazalishaji, wajasiriamali na taasisi za mafunzo ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania, kukuza ajira na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.


