CRDB YAUNGANISHA VIJANA NA FURSA ZA KIFEDHA RUKWA

Na Asha Mwakyonde, RUKWA

KONEKTI vijana na fursa za kifedha ili waweze kujitegemea kiuchumi ni miongoni mwa malengo ya Benki ya CRDB kupitia huduma na programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana, wakiwemo wanafunzi wa vyuo na wale wenye mahitaji maalumu.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Vijana Kitaifa yanayofanyika Sumbawanga mkoani Rukwa kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, benki hiyo inatoa elimu ya fedha na kutambulisha huduma zinazolenga kuwasaidia vijana kuweka akiba, kupata mitaji na kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Akizungumza leo Oktoba 9,2026 katika maonesho hayo, Meneja wa Mahusiano na Taasisi za Serikali wa Benki ya CRDB, Paskalina Diu, amesema benki hiyo imeamua kutumia maonesho hayo kuwafikia vijana na kuwapa elimu kuhusu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kufikia malengo yao.

Ameeleza kuwa kupitia kitengo cha vijana cha benki hiyo, CRDB imeandaa huduma zinazozingatia makundi na mahitaji tofauti ya vijana, kuanzia watoto hadi wanafunzi wa vyuo na vijana wanaojishughulisha na shughuli za ujasiriamali.

Amebainisha kuwa wanafunzi wa vyuo wanaweza kufungua akaunti ya Scholar, ambayo haina makato, huku wakipata fursa ya kunufaika na huduma ya mkopo wa awali wa fedha za kujikimu chuoni, unaojulikana kama ‘Boom Advance’.

Diu amesema huduma hiyo inamwezesha mwanafunzi kupata mkopo wa hadi asilimia 80 ya fedha za mkopo wa kujikimu anazotarajia kupokea kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ili kumsaidia kukidhi mahitaji yake wakati akisubiri fedha hizo.

Ameeleza kuwa fedha za mkopo huo zinapowasilishwa kwa mwanafunzi kupitia utaratibu wa bodi ya mikopo, hutumika kurejesha deni alilopatiwa awali, hatua inayolenga kupunguza changamoto za kifedha zinazoweza kuwakabili wanafunzi wanapoanza masomo.

“Ndiyo maana tupo hapa kuunganishwa na vijana, kwa sababu tunafahamu kuwa vijana wanaishi katika mazingira tofauti, lakini fursa zinapaswa kuwa sawa kwa wote, wakiwemo wanaoishi vijijini na wenye mahitaji maalumu,” amesema.

Awali Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Sumbawanga, Ruhore Masaka, amesema benki hiyo kupitia taasisi yake ya CRDB Foundation ina programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi, ikiwemo programu ya imbeJu

Amesema programu hiyo inalenga kuwasaidia vijana wenye mawazo ya biashara au ambao tayari wameanzisha shughuli za ujasiriamali kupata fursa za mitaji na huduma za kifedha zinazozingatia uwezo na mahitaji yao.

Masaka ameeleza kuwa akaunti ya imbeJu imeandaliwa kwa kuzingatia changamoto zinazowakabili vijana wanaoanza biashara, hasa wale ambao bado hawana uwezo wa kumudu makato na gharama mbalimbali za huduma za kibenki.

Amebainisha kuwa akaunti hiyo haina makato ya kila mwezi wala makato wakati wa kutoa fedha, huku vijana wanaokidhi vigezo vya programu wakipata fursa ya kuwezeshwa mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.

Ameongeza kuwa vijana wanaotaka kunufaika na huduma hiyo wanapaswa kuwa na kitambulisho kinachotambulika, kama vile kitambulisho cha Taifa au pasipoti, pamoja na kuwa na biashara au wazo la biashara linaloweza kutekelezwa.

Amesema lengo ni kuwasaidia vijana kuanzisha na kukuza biashara zao bila kuzidishiwa changamoto za kifedha katika hatua za mwanzo, ili waweze kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii.

Ushiriki wa Benki ya CRDB katika maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali na kuwapa taarifa kuhusu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia kutumia fursa zilizopo kujenga maisha bora kiuchumi.