Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
BENKKuu ya Tanzania (BoT) inatarajia kuzindua mfumo wa kidigitali utakaomuwezesha mtumiaji wa huduma za kifedha kuwasilisha malalamiko, kuanzia Januari mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 10,2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Ustawi wa Huduma Jumuishi za Kifedha, BoT, Nangi Massawe amesema jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya siku mbili kuhusu mfumo wa malalamiko kwa wawakilishi wa taasisi za fedha jijini Dar es Salaam.
“Mfumo umetengenezwa na kukamilika tunaamini ifikapo Januari katikati, tutauzindua rasmi ili wananchi waweze kutuma malalamiko yao, ni muhimu sana kwa kupitia warsha hii tuhakikishe wote tumeuelewa vizuri na kuanza kuutumia kabla ya kuuzindua.” amesema .
Alisema mfumo huo uliotengenezwa na kukamilika ni muhimu sana kwa watumiaji wa huduma za kifedha ambapo pia hautawaacha nyuma hata wale walio vijijini.
” Hivi tunavyozungumza watu wapo kazini kuhakikisha hata yule mwenye kitochi anaweza kutumia mfumo huu hivyo ni matarajio yangu kwamba kupitia warsha hii wote tunapata ueelewa mzuri na kuanza kuutumia kabla ya kuuzindua.”amesisitiza
Naye Kaimu Meneja Idara ya Ulinzi wa Fedha, (Financial Consumer Protection), Dkt. Khadija Kishimba, amesema BoT imeandaa warsha hiyo kwa taasisi za fedha ili kuuelewa mfumo kwani wao ndiowanaokutana na (walaji) wateja.
“Tunapaswa kuuelewa mfumo kwa sababu tunakwenda kusogeza huduma kwa walaji tunataka mwananchi alalamike kupitia kiganja chake.
“Ninyi ndio wenye mfumo, nasema hivyo kwasababu ninyi ndio mnaokutana na wananchi, BoT imeandaa mfumo na tunapopeleka automation kwenye taasisi za fedha sio lengo la BoT kubaki na mfumo huo, lengo letu wananchi watumie ili na sisi tupate mrejesho.” amesema.
Naye mtoa Mada juu ya Mfumo huo ambao utazinduliwa rasmi Januari mwakani Laura Mandari amesisitiza kuwa mfumo huo umeshakamilika takribani miezi miwili iliyopita na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni kujenga uelewa kwa Taasisi za Fedha na wananchi kwa ujumla.