DAS TEMEKE AZINDUA OFISI YA WILAYA YA KITANESCO YA MIKWAMBE

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Temeke Bw. Kimeta Mpui amezindua Ofisi mpya ya Wilaya ya KITANESCO Mikwambe ikiwa ni mkakati wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa kuendelea kuwahudumia na kusogeza huduma mbalimbali zinazotolewa na TANESCO karibu na wananchi.

Akizungumza Mei 16, 2026 wakati wa zoezi hilo amesema uzinduzi wa ofisi hiyo umelenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kutokana na mahitaji ya msingi ya Nishati ya umeme kwa wananchi yanavyozidi kuongezeka kila kukicha.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inaakisi maboresho ya kiutendaji yanayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto ya umbali kwa wananchi ambao hapo awali walilazimika kufuata huduma katika ofisi za Mkoa wa KITANESCO Kigamboni.

Amesema TANESCO imefanya mabadiliko makubwa ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya huduma ya umeme kutoka kwa wananchi hivyo ameipongeza TANESCO kwa kuanzisha ofisi hiyo nakuwataka wafanyakazi kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma bora zaidi kwa wananchi.

“Napenda kuupongeza uongozi wa TANESCO kwa kuanzisha ofisi hii kwani ni kielelezo cha maboresho ya kiutendaji inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza kero na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati”

Akizungumza Kaimu Meneja Huduma kwa Wateja, Bw. Shamu Lameck, amesema TANESCO imejipanga kikamilifu na inaendelea kuimarisha na kusogeza huduma zake kwa wateja ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za umeme.

“Hii ni sehemu mhimu sana, ni ishara kwamba TANESCO tumedhamilia kwamba hali ya upatiakanaji wa umeme Kigamboni unaimarika na huduma yenyewe pia,tumejipanga kuhakikisha kwamba wananchi na wateja wetu tunawahudumia kwa ukaribu na ubora zaidi.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni Mhandisi Paschal Luhavi amesema kuwepo kwa ofisi hiyo ya TANESCO Wilaya ya Mikwambe kunakwenda kusogeza huduma zaidi kwa wananchi ndani ya wilaya hiyo hasa maeneo ya kata za Kimbiji, Somangila, Pemba Mnazi na Kisarawe II na maeneo jirani.