Na Aziza Masoud,Dar es Salam
Benki ya Equity Tanzania imeanza programu ya darasa maaalum la mafunzo kwa ajili wafanyabiashara wadogo na wakati waliopo nchini kwa lengo la kuwasaidia kukuza biashara zao na kuwasaidia kupata mikopo benki.
Mafunzo hayo ya mwaka mmoja yatatolewa na benki hiyo kwakushirikiana na Kampuni ya ADC Tanzania pamoja na African Fund kupitia programu maalumu ya mafunzo ya elimu ya fedha na biashara kwa wafanyabiashara wanawake.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Meneja wa Mafunzo kutoka Benki ya Equity Tanzania, Martine Rajab amesema kutokana na uhaba wa elimu ya fedha na biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, wameamua kuanzisha darasa la mafunzo ya vitendo kwa watu 100 ambao wataanza nao kwa kipindi cha mwaka mmoja.
“Tutapita kwa mfanyabiashara mmoja baada ya mwingine, tukiendelea kumfundisha, ni kozi ya mwaka mzima, ambao lengo letu mtu huyu aweze kukopesheka na kumfundisha namna ya kupata masoko ndani na nje ya nchi”. alisema.
Alisema programu hiyo inalenga kuwasaidia wanawake kuongeza uwezo wao wa kibiashara, ikiwa ni pamoja na kuwa na vigezo vya kupata mikopo kupitia dawati la Mwanamke Plus lililoanzishwa kwa ajili ya biashara za wanawake.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ADC Tanzania, Esther Kitoka amesema ujio wa programu hiyo umetokana na tathimini iliyofanyika Afrika nzima na kuona kuna upungufu mkubwa wa mabenki kutoa mikopo kwa Wajasiriamali wadogo na wa kati hasa wanawake.
“Tunachoangalia zaidi ni kuhakikisha kwamba zile biashara zinakua, zinakuwa endelevu ili ziweze kurithishwa kwa vizazi na vizazi”. amesema
Aidha amesema wameona waingie katika eneo hilo wakishirikiana na wadau hao ili waweze kuhakikisha wanawasaidia wanawake waweze kukuza biashara zao na waweze kupata mikopo.
“Tutawafundisha kwa siku moja , baada ya hapo tutaenda kwa mmoja mmoja kwasababu changamoto zinapishana, wengine wanachangamoto za masoko, wengine changamoto ya uongozi, wengine katika kuweka mahesabu”,amesema
Amesema katika programu hiyo ya mwaka mmoja wanatarajia kuwafikia wanawake zaidi ya 100 katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar na kuweza kupata mikopo.
Kwa upande wake Mshiriki wa Mafunzo hayo Mjasiriamali, Cotrida Kagaruki amesema kupitia mafunzo hayo yatakwenda kuwasaidia namna ya kusimamia na kuratibu biashara zao.
Amesema wamefundishwa kuhusu utawala wa fedha, namna ya kusimamia mradi, kuwa na mipango mkakati na matumzi mazuri ya fedha ambazo watakuwa wanazipata.