Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WIZARA ya Katiba na Sheria imewahimiza Watanzania kutumia zaidi njia za mazungumzo ambayo inasaidia kuleta matokeo haraka kwa mfumo wa maridhiano katika kutatua migogoro badala ya kukimbilia mahakamani ambapo wanatumia muda mrefu kukamilisha taratibu za kupata haki zao.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba alipokuwa akitembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zilizo chini yake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo pia alishiriki kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi waliofika kupata ushauri.

Alisema wizara hiyo, kwa kushirikiana na taasisi zilizopo chini yake imeendelea kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu ya sheria pamoja na huduma za msaada wa kisheria.
“Tunaamini kwamba usuluhishi ni njia inayowafanya wale wenye migogoro waridhiane na kutoka wote wakiwa washindi, tofauti na mfumo wa mashauri mahakamani ambapo mara nyingi hupatikana mshindi mmoja na mwingine kushindwa,” alisema Katimba.

Alibainisha kuwa pamoja na mahakama kuwa na mamlaka ya kikatiba ya kusimamia upatikanaji wa haki, serikali inaamini kuwa njia mbadala za utatuzi wa migogoro zina mchango mkubwa katika kujenga maridhiano na kuimarisha mahusiano miongoni mwa wananchi.
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote wenye changamoto za kisheria kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili waweze kupata huduma za msaada wa kisheria,” alisema.

Mbali na hilo Katimba alisema Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 sambamba na kuanza kwa mwaka mpya wa bajeti 2026/2027, jambo linalohitaji mapitio makubwa ya sheria ili ziendane na malengo mapya ya maendeleo.
Alisema jukumu hilo linafanywa na Tume ya Marekebisho ya Sheria, ambayo imepewa dhamana ya kuhakikisha sheria za nchi zinaendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye.

“Kuna mabadiliko makubwa tunayotarajia kuyatekeleza kupitia Dira 2050, na mafanikio yake yanategemea uwepo wa sheria zinazowezesha utekelezaji wake,” alisema Katimba.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maendeleo ya teknolojia katika mchakato wa kutunga na kurekebisha sheria, akieleza kuwa Tanzania inaelekea kwenye uchumi unaotegemea mifumo ya kidijitali na matumizi madogo ya fedha taslimu.

“Tunapaswa kuhakikisha sheria zetu zinaendana na maendeleo ya teknolojia. Tunaelekea katika uchumi wa kidijitali na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kifedha, hivyo sheria lazima ziwezeshe mabadiliko hayo,” alisema.
Katimba pia alitembelea banda la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ambapo alipongeza juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki zao pamoja na kupokea maoni na maswali mbalimbali kutoka kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo.
Alisema ushiriki wa taasisi mbalimbali za wizara katika Sabasaba umeendelea kuwa daraja muhimu la kuwafikia wananchi na kuongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali katika sekta ya sheria na haki.


