KAPINGA:TEMESA MMEPIGA HATUA KUBWA KIDIGITALI

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ameipongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutengeneza magari pamoja na huduma mbalimbali wanazotoa kupitia vyombo vya moto vilivyopo chini yake na kusisitiza kuwa taasisi hiyo imepiga hatua  kwakuwa inaenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Kapinga ametoa kauli hiyo  Julai Mosi  alipotembelea  banda hilo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu  kama  Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Alisema  kwa naiba ya serikali anaipongeza TEMESA  kwa kasi ya mabadiliko inayoenda nayo katika matengenezo ya magari na mabadiliko ya mifumo ya utoaji huduma.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnazozifanya katika matengenezo ya magari na pia matumizi yenu ya mifumo katika utoaji huduma,hongereni sana,”alisema Kapinga.

Akiwa katika banda hilo Kapinga alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na TEMESA, ikiwemo huduma za vivuko, umeme na elektroniki, matengenezo ya magari na mitambo, ushauri wa kihandisi pamoja na mifumo ya kidijitali na ubunifu unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

TEMESA inaendelea kuwakaribisha wananchi, wadau na wageni wote kutembelea banda lake ili kujifunza kuhusu huduma zake, kupata ushauri wa kitaalamu na kufahamu mchango wa Wakala katika maendeleo ya sekta ya ufundi na umeme nchini.

Maonesho ya 50 ya biashara yanatarajiwa kufunguliwa rasmi  kesho Julai 3 na Rais wa Jamhuri ya  Msumbiji Daniel Chapo ambapo ataambatana na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Maonesho hayo ya biashara yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Hii ni Kubwa Kuliko” na yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya ijumaa tarehe 3 Juni, 2026