Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
KAMPUNI ya GASCO, kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), imesema katika mwaka wa fedha uliopita ilitekeleza miradi sita ya ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, ikiwemo kuwaunganishia huduma ya gesi wateja wapya wa viwandani na kibiashara.
Hayo yamesemwa leo Julai 2, 2026 na Mhandisi Mitambo wa GASCO, Daud Enock, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, ambapo amesema pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo, kampuni inaendelea kusimamia, kuendesha na kufanya matengenezo ya miundombinu yote ya gesi asilia inayomilikiwa na TPDC ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa uhakika.

Amesema miundombinu hiyo inajumuisha mitambo miwili ya kuchakata gesi asilia, ikiwemo uliopo Songosongo mkoani Lindi wenye uwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 140 za gesi kwa siku na mwingine uliopo Mtwara wenye uwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 210 kwa siku.
Ameeleza kuwa baada ya gesi kuchakatwa na kusafishwa, husafirishwa kupitia bomba la gesi hadi Kinyerezi, Dar es Salaam, ambako husambazwa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme, viwanda, taasisi na matumizi ya majumbani.

Enock amesema miongoni mwa watumiaji wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda mbalimbali, mitambo ya kuzalisha umeme, taasisi za umma pamoja na hoteli na majengo makubwa ya biashara.
Amesema GASCO pia inaendelea kuhakikisha miundombinu ya gesi asilia nchini inafanya kazi kwa ufanisi kupitia matengenezo, ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya pale miradi mipya inapopatikana.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili kampuni hiyo, amesema ni chache na kwa kiasi kikubwa zinahusisha taratibu za manunuzi, huku akieleza kuwa hazijazuia kampuni kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa GASCO itaendelea kuboresha huduma zake ili kuhakikisha miundombinu ya gesi asilia inaendelea kuwa salama, yenye kuaminika na kuchangia maendeleo ya sekta ya nishati pamoja na uchumi wa Taifa.


