Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limetumka Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu umuhimu wa mkondo wa amali unaotekelezwa katika shule za sekondari na kuwahamasisha wanafunzi kusoma masomk hayo ambayo yanatolewa kwa vitendo zaidi.
Akizungumza jana katika banda la NACTVET, Kaimu Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dora Tesha alisema baraza hilo lina jukumu kuu la taasisi hiyo ni kusimamia utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kuhakikisha yanatolewa kwa ubora katika shule mbalimbali.

“Mwaka huu pia wameamua kuonyesha mafanikio ya mkondo wa amali ulioanzishwa kupitia maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023.
Alisema lengo la mkondo huo ni kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kazi tangu wakiwa shule za sekondari ili wanapomaliza kidato cha Nne wawe tayari kujiajiri au kuendelea na masomo ya kitaaluma wakiwa tayari na ujuzi wa vitendo.

“Tumewaleta wanafunzi kwenye maonesho haya ili wazazi, walezi na wananchi waone kwa vitendo uwezo wao. Wapo wanafunzi wa umeme, ujenzi na fani nyingine wanaoweza kufanya kazi ambazo zamani zilitarajiwa kufanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu,” alisema.
Naye Careen Jonathan ambaye ni wanafunzi wa Kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Baobab ambaye anasoma mkondo wa amali alisema mfumo huo umemsaidia kupata ujuzi wa umeme na kushiriki kuandaa miradi mbalimbali ya vitendo.

Alisema mfuml wa amali unawapa wanafunzi nafasi ya kuchagua taaluma zinazowasaidia kutimiza ndoto zao za baadaye, zikiwemo uhandisi na fani nyingine za kiufundi.
“Naiomba Serikali iendelee kuimarisha na kusambaza mfumo huu katika shule nyingi zaidi ili wanafunzi wengi wanufaike na nchi ipate wataalamu wenye ujuzi,” alisema.

Kwa upande wake Daudi Elias ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Wavulana Bwiru alisema ambaye anajifunza somo la amali la ujenzi alisema kupitia mafunzo hayo ameweza kujifunza kuchora ramani za majengo na kubuni nyumba za gharama nafuu zinazoweza kujengwa na wananchi wanaoanza maisha.
“Mfumo huu ni mzuri utatusaidia kujiajiri,mfano mimi najifunza uandisi wa majengo,hiyo ni kujenga kila kiti nimekuja hapa na mfano wa nyumba ya mtu anayeanza maisha ambayo ina vyumba viwili,”alisema.

Naye mwalimu wa taaluma ya amali katika Shule ya Sekondari Baobab, Philip Razalo, alisema mkondo huo unawajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri na kutengeneza ajira badala ya kusubiri kuajiriwa.
Alibainisha kuwa shule hiyo ina wanafunzi 77 wa mwaka wa kwanza, 28 wa mwaka wa pili na 30 wa mwaka wa tatu katika mkondo wa amali, jambo linaloonyesha ongezeko la mwitikio wa wanafunzi.
Pia aliiomba Serikali kuongeza uwekezaji katika karakana na vifaa vya kufundishia, kuhakikisha upatikanaji wa vitabu vya rejea pamoja na kuandaa walimu wenye ujuzi wa kufundisha masomo ya amali kwa ufanisi.


