WAZIRI WA FEDHA AIPONGEZA IAA KWA KUWAJENGEA UWEZO WA UJASIRIAMALI WAFUNGWA

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameipongeza Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA) kwa kuanzisha programu za mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara zinazolenga makundi maalumu, ikiwemo kuwajengea uwezo wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo vyao ili waweze kujitegemea wanaporejea katika jamii.

Pongezi hizo alizitoa Julai 2, 2026, alipotembelea banda la IAA katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, yanayoshirikisha taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Fedha.

Akitoa maelezo kwa Waziri huyo, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa, Uhusiano na Masoko wa IAA, Sarah Goroi, alisema kwa sasa taasisi hiyo ina kampasi sita zilizopo Arusha, Dodoma, Babati, Songea, Dar es Salaam na Bukombe, huku ikitarajia kufungua kampasi Zanzibar ifikapo Oktoba mwaka huu.

Alisema IAA ina wanafunzi takribani 25,000 na inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kutekeleza programu za mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara kwa makundi maalumu.

Goroi alitaja miongoni mwa taasisi zinazoshirikiana na IAA kuwa ni Jeshi la Magereza, ambapo mafunzo hayo hutolewa kwa wafungwa wa Gereza la Ukonga wanaokaribia kumaliza vifungo vyao, kwa lengo la kuwapatia ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kujipatia kipato halali watakaporejea uraiani.

Alifafanua kuwa mafunzo hayo hutolewa ndani ya kipindi cha miezi sita kabla ya wafungwa hao kuachiwa huru, ili kuwaandaa kuanza maisha mapya yenye kujitegemea na kupunguza uwezekano wa kurejea tena gerezani.