DIB YALIPA BILIONI TISA KWA WALIOKUWA WATEJA WA BENKI ZILIZOFUNGWA

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

BODI ya Bima ya Amana (DIB), imesema mpaka sasa jumla Sh Bilioni tisa kati ya Bilioni 11 zimeshalipwa kwa wateja waliokuwa wamehifadhi fedha katika benki saba  zilizotangazwa mufilisi na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)   kuwasisitiza wateja kufika katika benki walizotangaziwa kuchukua fedha zao.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam,Afisa Mwandamizi  DIB  Silvan Makore alisema fedha hizo zinalipwa kupitia benki ambazo zimepewa kandarasi za kusimamia malipo hayo   DIB  kutokana na bodi hiyo kutokuwa na matawi katika maeneo mengi.

“Kuna benki tuliziteua kwa ajili ya wateja wanaoidai bima ya amana,wateja ambao walihifadhi fedha zao katika benki zilizofilisiwa kamaa benki ya biashara TCB inalipa wateja wanaodai bima ya amana,tuliona DIB ni busara ili mwananchi asipande gari akitumia fedha nyingi kupata fedha zake kwajuja kwenye matawi yetu yaliyopo Dar es Salaam na Dodoma.

“Mteja akifika benki husika atatoa kitambulisho  atatambuliwa na wafanyakazi wa TIB atajazishwa fomu na kulipwa fedha zake pia wateja waliokopa kwenye  benki zilizofungwa wanalipa malipo yao kupitia NMB kwakuwa benki ipo nchi nzima ,”alisema  Makore.

Alisema  kati ya  benki saba zilizofungwa 2018 kiwango cha fidia kilikuwa Sh bilioni 11  na mpaka sasa wameshalipa Sh Bilioni tisa  sasa zimebaki bilioni tatu hazijachukuliwa  na wateja.

Alisema fedha hizo zilizobaki ni nyingi hivyo wateja waliokuwa kwenye benki hizo ni vyema wakaenda kuzichukua kwakuwa ikifika miaka 15  hazijachukuliwa  zinarudishwa serikalini

Akizungumzia kuhusu usalama wa fedha kwa wateja  katika  baadhi ya benki  Makore aliwatoa wasiwasi wananchi ambao wanahofia kuhusu fesha zao na kusisitiza kuwa kila benki inalipa  kiasi cha fedha DIB kwa ajili ya ulinzi wa fedha za wateja.

“Ukiwa mteja wa benki wewe ni mteja wa bima ya amana ukiweka pesa benki ujue huko  unalipiwa  hata ikitokea Benki Kuu ikafungia benki yako unapaswa kujua kuwa  upo salama.

“Na sisi kila baada ya miezi tunahakikisha wanakuja kuleta ripoti yao ya ukaguzi  uendeshaji wa robo   mwaka au mwaka mzima tuone kama benki yako inapata faida au hasara,hata mteja una wajibu wakufuatilia ripoti hizo na ukiona mwenendo sio mzuri unafumgua akaunti benki nyingine,”alisema Makore.

Alisema mteja pia una uwezo wakuhoji  kwa nini benki husika wamepata hasara  na wahusika watatoa sababu na watakwambia jitihada wanazofanya kuongeza faida.

Amewataka  wananchi ambao hawana uelewa wa  masuala ya amana za benki kufika katika banda hilo kupatiwa elimu hiyo.