MHE. NDEJEMBI ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA KITUO CHA UMEME IGANJO, MBEYA

📌 Ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 93 ya utekelezaji

📌 Aeleza manufaa ya mradi katika kuchochea shughuli za uchimbaji madini, uwekezaji viwandani na kuongeza fursa za ajira

Na Mwandishi Wetu,Mbeya

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Iganjo mkoani Mbeya, ambacho ni sehemu ya Mradi wa Tanzania–Zambia Transmission Interconnector (TAZA), unaolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia.

Mhe. Ndejembi ameeleza hayo leo, Oktoba 16, 2026, alipotembelea kituo hicho ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme nchini.

Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa, hatua itakayochochea shughuli za uchimbaji madini, ukuaji wa viwanda, uwekezaji na kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana, pamoja na kuwezesha usafirishaji wa umeme kwenda nchi jirani ikiwemo Zambia.

“Umeme utakaofika hapa si kwa ajili ya nchi jirani ya Zambia pekee, bali pia utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa. Naipongeza sana Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kazi nzuri iliyofanyika. Nilipofika hapa mwezi Machi, mradi ulikuwa katika hatua za awali, lakini kwa sasa uko mbioni kukamilika. Kwa maendeleo haya, nimeridhika na nilichokiona,” amesema Mhe. Ndejembi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuimarisha upatikanaji wa umeme na kufungua fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ameeleza kuwa Kituo cha Iganjo kitakuwa na uwezo wa kusafirisha umeme kwenda maeneo yenye mahitaji makubwa ya nishati, ikiwemo Saza mkoani Songwe, ambako shughuli za uchimbaji madini zinahitaji umeme wa uhakika, pamoja na kuwezesha usafirishaji wa umeme kwenda nchi jirani ya Malawi.

“Kazi hii inafanyika kwa kasi kubwa kutokana na umuhimu wake katika maendeleo na kufungua fursa za kijamii na kiuchumi. Kituo hiki cha Iganjo pia kitakuwa na uwezo wa kupeleka umeme katika eneo la Saza mkoani Songwe, ambako kuna uhitaji mkubwa wa umeme kwa shughuli za uchimbaji madini, pamoja na nchi jirani ya Malawi,” amesema Mhe. Makamba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema ujenzi wa Kituo cha Iganjo unaogharimu takribani shilingi bilioni 175 umefikia asilimia 93, huku kituo hicho kikitarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na maeneo jirani.

“Mradi huu una umuhimu mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Uyole, Mbarali, Tukuyu na Busokelo, kupitia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme,” amesema Bw. Twange.

Aidha, ameeleza kuwa ifikapo Desemba 5, 2026, Kituo cha Iganjo kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kupokea umeme unaozalishwa katika Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), kufuatia kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Zuzu mkoani Dodoma hadi Tagamenda mkoani Iringa.

Mradi wa TAZA, unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga mkoani Rukwa, unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi trilioni mbili, ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo na kuwezesha biashara ya umeme kati ya Tanzania na nchi jirani.