Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewaalika wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyopo jijini humo kukutana naye Novemba 14, 2026, kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kuzitatua.
Chalamila ametoa mwaliko huo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akieleza kuwa mkutano huo utafanyika katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Amesema mkutano huo utakuwa fursa kwa wanafunzi kupata ushauri na maelekezo kuhusu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika masuala yao ya kielimu na kijamii.
Aidha, amesema katika mkutano huo watakuwepo wawakilishi kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ili kusaidia kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za wanafunzi.
Chalamila amebainisha kuwa Serikali kupitia HESLB imeendelea kugharamia wanafunzi wengi wa elimu ya juu, huku akitambua kuwa baadhi yao wamekuwa wakifika mara kwa mara katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba msaada kuhusu changamoto mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo, amesema ameamua kuwakutanisha wanafunzi hao pamoja na taasisi husika ili waweze kueleza changamoto zao na kupata ufumbuzi kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na viongozi pamoja na watendaji wa taasisi hizo.
Mkutano huo unatarajiwa kuwapa wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam nafasi ya kuwasilisha changamoto zao na kupata ufafanuzi kutoka kwa taasisi zinazohusika.


