Na Mwandishi Wetu,Mtwara
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, leo amewasili mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku tano huku akiwataka wanachama wa chama hicho kuwa madhubuti kushikamana, kupendana,kushirikiana na kutambua kuwa wanawajibu wa kuwatumikia watanzania kwa nguvu zote.
Hayo ameyasema leo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Masasi,amesema CCM inaamini umoja na utulivu unategemewa sana na chama hicho katika kuwa madhubuti.
Amesema wana CCM wanawajibu wa kupata viongozi wazuri ambao wanamoyo wa kuwatumikia wananchi..”wale wazuri miongoni mwetu wapewe nafasi ya kuongoza kwenye jamii.
“Wana CCM wanajukumu la pekee la kuchujana kuhakikisha wanapata viongozi wazuri ambao wanapata nafasi ya kuongoza jamii ambao tunategemea tukiwapa heshima hiyo wataleta heshima ya CCM na nchi yetu ,”amesema.
Dkt.Nchimbi amefurahishwa na umoja waliouonyesha wana CCM wa Masasi kwa namna walivyojitokeza kwa wingi katika mapokezi yake.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu wa CCM ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa-NEC, Oganaizesheni, Issa Usi Haji Gavu, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA- Amos Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa-SUKI- Rabia Hamid Abdalla.