TANESCO:WANANCHI MSIHOFU KUTUMIA NISHATI YA UMEME KATIKA VYOMBO VYA USAFIRI

MD Twange asema TANESCO inajenga vituo vya kuchajia vyombo hivyo nchi nzima

Aeleza mpango wa kusambaza majiko sanifu ya umeme takribani Mil 1

Awapongeza Wafanyakazi kwa ubunifu na jitihada za kuwahudumia wateja kwa ufanisi.

Na Mwandishi Wetu,Dodoma

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amewaondoa hofu wananchi kuhusu matumizi ya nishati ya umeme katika vyombo vya usafiri, akisema kuwa TANESCO imejipanga kujenga vituo vya kuchajia vyombo hivyo nchi nzima.

Mkurugenzi huyo amesema hayo Juni 19, 2026, alipotembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali, mkoani Dodoma.

Amesema shirika linatambua kuwa mahitaji ya umeme yanaendelea kuongezeka kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi, hivyo jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kwa ubora na uhakika kwa matumizi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

“TANESCO inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Aidha, sasa tunashuhudia matumizi ya umeme katika vyombo vya usafiri. Sisi kama wazalishaji wa umeme tunaonesha njia kwa kuwa tuna vyombo vingi vya usafiri vinavyotumia umeme. Tumejipanga kujenga vituo vya kuchajia vyombo hivyo nchi nzima,” alifafanua Bw. Twange.

Bw. Twange pia amefafanua kuhusu mpango wa ukopeshaji wa majiko sanifu ya umeme kwa wananchi, unaowawezesha kulipa kidogo kidogo kupitia manunuzi ya Luku. Amesema kuwa, kwa kushirikiana na wadau , takribani majiko milioni 1 yatasambazwa katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu.

“Tunatumia mbinu mbalimbali kuwaelimisha wananchi na kuwaondoa hofu kuhusu matumizi ya umeme kupikia. Tunawakopesha majiko ya umeme na wanalipa kidogo kidogo kupitia mfumo wa manunuzi ya Luku. Wadau kutoka sekta binafsi wametuunga mkono, na tunatarajia kusambaza majiko karibu milioni 1 katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu,” aliongeza Bw. Twange.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi. Beatrice Kimoleta, Licha ya kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kutembelea Banda la TANESCO kujionea namna wananchi wanavyohudumiwa, amesema Shirika linajivunia watendaji wenye dhamira ya kuwahudumia wananchi kwa ubunifu na weledi mkubwa.

“Tunaomba wateja wetu muendelee kutuamini, Tunafahamu kuwa umeme ni huduma muhimu kwa kila Mtanzania, hivyo tunaendelea kuongeza jitihada za kutoa huduma bora, ya uhakika na yenye ufanisi zaidi, tunaimani na watumishi wetu katika kuhakikisha wananchi wananufaika na nishati ya umeme katika fursa mbalimbali ,” alisisitiza Bi. Kimoleta.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa kwa mwaka 2026 yanaendelea kufanyika katika Viwanja vya Chinangali, mkoani Dodoma, na yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi Juni 23, 2026.