EWURA CC YAWATAKA WANANCHI KUHAKIKI BILI ZA MAJI

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) limewataka watumiaji wa maji kuhakiki bili pamoja na wa mafuta kuhakikisha bei za mafuta kila zinapotangazwa.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji Mwandamizi wa EWURA CCC, Lugiko Lugiko alisema watumiaji wa huduma za nishati wanapaswa kuwa makini katika kufuatilia  huduma za maji.

Alisema wananchi wanapaswa kuhakiki usomaji wa mita na kuchunguza uwepo wa uvujaji wa maji kabla ya kulalamikia bili kubwa.

“Kabla hatujaanza kulalamika kuhusu kuhusu masuala ya bili lazima ufuatilie,changamoto nyingi husababishwa na hitilafu zinazoweza kuzuilika.

Alisema pia  watumiaji wa mafuta wanapaswa  kuhakiki bei rasmi zinazotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuhakikisha pampu inaanzia sifuri wakati wa kujaza mafuta na kudai risiti kama ushahidi wa manunuzi, huku akisisitiza kuepuka kununua mafuta katika vituo visivyo na leseni.

Mbali na hilo amewahimiza Watanzania kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme na gesi, akisema matumizi yake ni salama, yanaokoa muda na yanachangia kulinda mazingira pamoja na kuboresha afya za wananchi.

 Alisema wananchi wanapaswa kupata elimu kwa watumiaji wa huduma za maji, umeme, mafuta na gesi  kwakuwa ni njia muhimu ya kupunguza bili zisizo za lazima, kuimarisha usalama na kuhakikisha wananchi wanatambua haki na wajibu wao wanapotumia huduma hizo.

Amesema baraza hilo linatumia maonesho hayo kuwafikia wananchi kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma za nishati na maji.

“Tunatoa elimu kwa wananchi ili wawe watumiaji wenye taarifa sahihi, kwa sababu mtumiaji anayefahamu haki na wajibu wake ana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuepuka gharama zisizo za lazima,” amesema Lugiko.

Ameongeza kuwa watumiaji wa umeme wanapaswa kutumia mafundi wenye leseni ya EWURA, kufunga vifaa vya viwango vinavyokubalika na kufanya ukaguzi wa miundombinu ya umeme mara kwa mara ili kupunguza matumizi makubwa ya umeme pamoja na kuepusha ajali.