Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limesema elimu ya amali na mafunzo ya ufundi ndiyo nguzo muhimu ya kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi itakayochochea ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katibu Mtendaji wa NACTVET, Mwajuma Ibrahim Lingwanda, alisema vijana wanaopata elimu ya amali na ufundi hujengewa uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo, kujiajiri, kuajiriwa na kubuni teknolojia zinazochangia maendeleo ya nchi.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) leo Julai 6, 2026 Lingwanda alisema moja ya vivutio katika banda la NACTVET mwaka huu ni wanafunzi wa shule za amali wanaoonesha ujuzi wao kwa vitendo kupitia kazi mbalimbali walizojifunza.
“Vijana hawa wanaonyesha kwamba kile wanachojifunza darasani wanakiweka kwenye vitendo. Hii ndiyo aina ya nguvu kazi ambayo Taifa linaihitaji ili kuongeza uzalishaji, ubunifu na ushindani wa bidhaa za Tanzania,” alisema.
Alisema NACTVET imetumia maonesho hayo kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutoa ushauri kuhusu uanzishaji wa taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na baraza hilo.

Lingwanda alisema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, jambo linaloonesha kuwa jamii inaendelea kutambua umuhimu wa elimu ya ufundi katika maendeleo ya kiuchumi.
Aliwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika shule zinazotoa elimu ya amali ili kuwajengea ujuzi unaowawezesha kujitegemea na kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.

Pia aliwataka wawekezaji na wadau wa elimu kuanzisha shule na taasisi zinazotoa mafunzo ya amali, akisema NACTVET ipo tayari kutoa mwongozo kuhusu taratibu za usajili na uendeshaji wa taasisi hizo.
Kwa mujibu wake, ongezeko la bidhaa zinazozalishwa nchini na kuoneshwa katika Maonesho ya Sabasaba linaonesha kuwa Tanzania inaendelea kujenga uchumi unaotegemea uzalishaji na ujuzi wa wananchi wake, hatua inayochangia kuongezeka kwa ajira na ukuaji wa viwanda.




