Prof. Mbarawa azindua jengo la muda la abiria kiwanja cha ndege Songea

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amezindua jengo la muda la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Songea mkoani Ruvuma chenye uwezo wa kuhudumia abiria 300 kwa wakati mmoja.

Prof.Mbarawa amefanya uzinduzi huo katika siku ya kwanza ya ziara ya siku nne mkoani Ruvuma ambapo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kitembelea mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza katika hafla hiyo Prof.Mbarawa amesema kuwa pamoja na ujenzi wa jengo hilo la muda serikali inakusudia kujenga jengo la kudumu ili kuendana na hadhi ya uwanja huo wenye uwezo wa kufanya kazi saa 24.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tumesikia mobile lako tutaongeza safari za ndege Ruvuma sasa ziko nne kwa wiki lakini tutaongeza zaidi kila wakati itakapohitajika, tunaamini kufanya hivyo tutachochea uwekezaji, biashara na utalii kwa kuwaunganisha wananchi na fursa za maendeleo,” Amesema Mbarawa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mohammed Abbas amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuistawisha Ruvuma na kumpongeza Waziri Mbarawa kwa kuhakikisha ujenzi wa kiwanja na miundombinu yake vinakamilika kwa wakati na kwa ubora.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo, Mkurugenzi wa Uhandisi na Huduma za Kiufundi Focus Kadeghe amesema Kiwanja cha Ndege cha Songea ni miongoni mwa viwanja 61 vinavyosimamiwa na kuendelezwa na TAA, kikiwa lango muhimu la usafiri wa anga kwa Mkoa wa Ruvuma na ukanda wa Kusini mwa Tanzania.

Kadeghe amesema kuwa Serikali imetekeleza mradi mkubwa wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya kiwanja hicho uliohusisha uboreshaji wa njia ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, maeneo ya usalama, uzio wa kiwanja, mitaro ya maji ya mvua, barabara za ndani, taa za kuongozea ndege, vifaa vya mawasiliano ya anga, jengo la mitambo ya nishati, mnara wa muda wa kuongozea ndege, pamoja na ununuzi wa gari la kisasa la zimamoto.

Aidha ameongeza kuwa mradi wa ukarabati wa jengo hilo ulianza Oktoba 15, 2024 kwa kutumia mapato ya ndani ya TAA na kutekelezwa na Kampuni ya Wesons Engineering Ltd na limekamilika pamoja na ujenzi wa barabara ya ndani na maegesho ya magari yenye uwezo wa kuhudumia magari 100 kwa wakati mmoja, kwa gharama ya shilingi milioni 842.37.