Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) imesema wilaya ya Temeke ina watu 2500 wanaotumia dawa tiba za methadone kutokana na matumizi ya heroin jambo linalosababisha wilaya hiyo kuongoza kwakuwa na waraibu wengi mkoan Dar es Salaam.
Akizungumza katika tamasha la kupinga dawa za kulevya lililofanyika viwanja vya Mwembe Yanga Temeke kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo ,Kamishna Divisheni ya Kinga,Tiba na Huduma na Utengemao Dk.Cassian Nyandindi amesema wilaya ya Temeke inaongoza kwakuwa na watu waliopata tatizo ya uraibu kwa mkoa wa Dar es Salaam huku wilaya za Kinondoni,Ilala,Ubungo na Kigamboni zikifuata.

“Tatizo la dawa za kulevya ni kubwa kwa Dar es Salaam kwa wilaya zote lakini wilaya ya Temeke inaongoza kwakuwa katika eneo hili tatizo ni kubwa kwakuwa watu 2500 waliokuwa wakitumia dawa za kulevya aina ya heroin wanatumia huduma ya methadone,idadi hiyo ni idadi kubwa kiwilaya,”alisema Dk.Nyandindi.
Alisema mbali na kutumia methadone pia waraibu 16000 wamepatiwa huduma ya tiba ya tibiwaafya ya akili kwa wilaya ya Temeke kwa mwaka 2014.
Alisema kutokana na hali hiyo matamasha hayo ni muhimu kwakuwa yanasisitiza uwepo wa tatizo la dawa za kulevya na kwamba si jambo la mtu mmoja bali ni la jamii nzima.

“Ninachopenda kusisitiza ni kwamba tatizo la dawa za kulevya haliwezi kumuacha mtu salama,kama halitakugusa mtu binafsi litamgusa mwanafamilia majirani na jamii kwa ujumla,sisi sote tunatakiwa kupiga vita dawa za kulevya,kila mwaka DCEA uhamasisha kushiriki kupambana na dawa za kulevya,”alisema Dk.Nyandindi.
Alisema matamasha hayo pia hufanyika kikanda ambapo kuna kanda ya Mashariki,kanda ya ziwa na Nyanda za Juu Kusini na Mtwara pamoja na Kanda ya Kusini.

Naye Mkuu wa wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda ambaye alikuwa mgeni rasmi wa ghafla hiyo alisema wilaya hiyo imekuwa na idadi kubwa ya waraibu wa madawa ya kulevya kutokana na haiba ya watu wa eneo hilo.
“Temeke ni rahisi sana kutumika katika matumizi na usambazaji,jiografia yetu na mazingira ni rafiki sana kwenye kusambaza na kutumia,kutuletea ghafla hii Temeke ni fursa ya watu kupata elimu.
“Kuna watu wapo wamezunguka wanasikiliza hapa inaonyesha namna gani suala hili la madawa ya kulevya ni seriuos nchini,bahati mbaya maangamizi yake ni ya muda mrefu watumiaji wanakutana tu matokeo ambayo kupona kwake sio rahisi,”alisema Mapunda.

Alisema ni muhimu kupambana na madawa ya kulevya katika ngazi zote lakini pia jamii ikitaka kumaliza kabisa dawa zakulevya kwa njia rahisi kukata mnyororo wa usamabazaji ambayo ni ngumu kwakuwa unawaza unaanzia wapi kwenye kiwanda kusafirisha au yanapohifadhiwa.
“Kuna ugumu wakukata supply kwa sababu haina njia moja wala formula moja,la pili kupambana na yule anayeenda kutumia kwakuwa tusipokuwa na watumiaji mzigo hautafika,tukikata watumiaji mzigo hautafika mtaani kwa sababu utakuwa hauna soko,”alisema Mapunda.

Alisema kutokana na mapambano la tatizo hilo kuwa kubwa ni wakati wa wazazi kuongea na watoto wao mapema kuhusu dawa za kulevya na madhara yake ili kupunguza wimbi la watumiaji.
“Watoto wanapaswa kuambiwa sio kila jambo ni la kujaribu,vitu havijaribiki wala wasionje kwa sababu vitawapeleka sehemu ambayo hawatoweza kutoka wala kurudi nyuma,”alisema Mapunda.

Naye mmoja wa waraibu ambaye amepata nafuu na kuanzisha kituo Sura Nyembo alisema alianza kutumia dawa za kulevya aina ya heroin mwaka 2000 na kuacha mwaka 2013 kupitia nyumba za kujitibu.
“Nimetumia heroin kwa miaka 13 kupitia nyumba hizi za kujitibu nilibahatika kuondokana na matumizi haya,jamii inatakiwa kujua madawa ya kulevya sio kitu kizuri,mimi niliacha hadi masomo,”alisema Nyembo.

Alisema ili kuondoa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya kuna haja kuhakikisha watumiaji wanapungua ili kupunguza uhitaji utakaoondoa usamabazaji.
Alisema pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya kuenea pia kwa sasa kumekuwa na wimbi la watu wanaotumia bangi aina ya skanka.


