Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAANDISHI wa habari nchini wanaoshiriki Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma ni miongoni mwa kundi linaloongoza kwa kujitokeza kukata bima za maisha, hatua inayotajwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu wa huduma hiyo
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa NIC Insuarance, Karimu Meshack, alisema waandishi wa habari wameonyesha mfano kwa kuchukua bima za maisha na ajali, akiwataka Watanzania wengine kuiga hatua hiyo.

Alisema taaluma ya uandishi wa habari, kama zilivyo kazi nyingine, inakabiliwa na hatari mbalimbali, hivyo ni muhimu kwa wahusika kuhakikisha familia zao zinakuwa na kinga ya kifedha endapo watapatwa na matatizo au kupoteza maisha.
“Mwandishi wa habari anaweza kuwa nyuma ya kamera, mbele ya kipaza sauti au akiandika habari kila siku. Lakini kesho haijulikani. Akishindwa kufanya kazi au akifariki, familia yake itaishije? Ndiyo maana tunasisitiza umuhimu wa bima za maisha,” alisema.

Meshack alisema lengo la bima za maisha ni kulinda kipato cha familia kwa kuhakikisha wategemezi hawaathiriki kifedha endapo mteja atapatwa na janga.
Mbali na bima za maisha, alisema shirika hilo linaendelea kutoa elimu kuhusu bima za kilimo, mifugo, mali na ajali ili kuwasaidia wananchi kulinda uwekezaji wao dhidi ya majanga kama ukame, mafuriko, magonjwa, moto, wizi na ajali.

Alisema kuongezeka kwa matumizi ya bima kutasaidia kulinda uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kuimarisha uchumi wa taifa.
Aidha, alisema NIC imeboresha upatikanaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kidijitali ikiwamo programu ya simu, tovuti na huduma za WhatsApp, hatua inayowezesha wananchi kununua bima, kufungua madai na kufuatilia mwenendo wake bila kufika ofisini.
Meshack alisema madai yasiyohitaji uchunguzi hulipwa ndani ya siku saba, huku akiwahimiza wananchi kutumia huduma za bima kama sehemu ya kupanga maisha yao ya sasa na baadaye.


