WAZIRI KAIRUKI AITAKA TTCL KUONGEZA KASI YAKUUNGANISHA FIBER MAJUMBANI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Kairuki, ameitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza kasi ya kuwaunganisha wananchi na intaneti ya mkongo wa nyuzi majumbani (FTTH), huku akilenga huduma hiyo kuwafikia nyumba milioni moja ifikapo Juni 2028.

Kairuki alitoa agizo hilo leo Agosti 21, 2026 ,jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi awamu ya pili ya mradi wa “Fiber Mlangoni Kwako”, unaolenga kuongeza upatikanaji wa intaneti yenye kasi na uhakika nchini.

Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa kidijitali, ikizingatiwa kuwa intaneti ya kasi inawaunganisha wananchi na fursa za elimu, ajira, biashara, ubunifu na huduma mbalimbali.

“Fiber si waya tu unaofika nyumbani au ofisini, bali ni daraja muhimu linalomuunganisha mwananchi na fursa za uchumi wa kidijitali,” alisema Kairuki.

Alisema takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo mwaka iliyoishia Juni 2026 zinaonyesha kuwa usajili wa intaneti nchini ulifikia milioni 62.7, huku matumizi ya data yakifikia petabytes 1,041.

Hata hivyo, alisema idadi ya watumiaji wa huduma ya fiber majumbani bado ni ndogo, ikiwa ni 178,904 pekee.

Kairuki alisema hali hiyo inaonyesha kuwa pamoja na ongezeko la matumizi ya intaneti, bado kuna pengo kubwa katika upatikanaji wa huduma ya fiber kwa kaya.

Alisema awamu ya pili ya mradi huo inalenga kuongeza home passes hadi 500,000, kabla ya kufikisha milioni moja ifikapo Juni 2028.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa mafanikio ya mradi huo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya nyumba ambazo nyuzi zimefika pekee, bali pia kwa idadi ya wateja wanaounganishwa, ubora wa huduma, kasi ya intaneti, gharama na muda wa kutatua hitilafu.

“Hatupaswi kuridhika na fiber kupita mbele ya nyumba ikiwa kaya haiwezi kujiunga. Hatupaswi kuridhika na usajili ikiwa huduma haitimizi ahadi ya kasi na uhakika,” alisema.

Kairuki aliitaka TTCL kuipa kipaumbele maeneo yanayokua kwa kasi, vituo vya biashara, masoko, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, alitaka kurahisishwa kwa taratibu za usajili na kupunguzwa kwa muda wa kuunganisha huduma, huku akitaka TTCL kushirikiana na serikali za mitaa, waendelezaji wa makazi, wamiliki wa majengo na jumuiya za wafanyabiashara.

Katika kuboresha huduma kwa wateja, Waziri huyo aliitaka TTCL kuimarisha ufuatiliaji wa mtandao, matengenezo ya kinga na urejeshaji wa huduma kwa haraka.

Alisema mteja anayewasilisha malalamiko hapaswi kuachiwa jukumu la kufuatilia tatizo lake, bali shirika linapaswa kumjulisha hatua zilizofikiwa hadi changamoto hiyo itakapopatiwa ufumbuzi.

Pia, alilitaka shirika hilo kubuni vifurushi vinavyomudu makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi, vijana, wafanyakazi, wavuvi, wachimbaji, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na taasisi.

“Gharama za kuunganisha huduma, vifaa na vifurushi hazipaswi kuwa kikwazo,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Abubakar Asenga, alishauri Serikali kuongeza uwekezaji na bajeti kwa TTCL ili kuwezesha upanuzi wa huduma hiyo.

Asenga alisema Bunge kupitia kamati hiyo limekuwa likisisitiza kuimarishwa kwa TTCL ili iwe chombo muhimu katika kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi na kuongeza mapato ya Taifa.

Alisema ushauri wa kukabidhi TTCL jukumu la kusimamia shughuli hiyo umeanza kuonyesha matokeo, akieleza kuwa hadi mwaka wa fedha 2024/25, shirika hilo lilikusanya takribani Sh100 bilioni kutokana na kuunganisha wateja wapatao 280,000.

Kwa mujibu wa Asenga, mpango ni kuongeza mapato hadi Sh400 bilioni ifikapo 2029 baada ya kuunganisha wateja milioni moja.

Alisema iwapo idadi ya wateja itafikia milioni mbili, shirika linaweza kufikia mapato yanayokaribia Sh1 trilioni ifikapo 2030.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema awamu ya pili ya mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kibiashara wa miaka 10 wa shirika hilo unaoanzia mwaka 2025/26 hadi 2034/35.

Marwa alisema mpango huo unalenga kuboresha huduma, kuongeza wateja na mapato, kuimarisha uendeshaji wa kielektroniki pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Alisema TTCL imeanza kutumia teknolojia ya GPON, inayowezesha kutoa intaneti yenye kasi kubwa, kuunganisha wateja wengi kwa wakati mmoja na kupunguza gharama za uendeshaji.

Alisema awamu ya kwanza ya mradi ilitekelezwa katika Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Mbeya, Mwanza na Unguja Zanzibar, ambako takribani home passes 38,000 zilijengwa.

Marwa alisema utekelezaji wa awamu ya pili ulianza Julai 2026 na unatarajiwa kujenga jumla ya home passes 400,000.

“Mpango huu utapelekea takribani maunganisho 750,000 kuwa yamejengwa kufikia Juni 2027, na mpango wa Shirika ni kufikia maunganisho takribani milioni moja ifikapo Juni 2028,” alisema.

Alisema upanuzi huo unatarajiwa kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali nchini.