Na Mwandishi Wetu,Rufiji
TANZANIA imeingia katika hatua mpya ya uzalishaji na matumizi ya nishati baada ya kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaotarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea uwekezaji, viwanda na biashara ndani na nje ya nchi.
Mradi huo umeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuiwezesha Tanzania kuwa na ziada ya nishati, hali inayofungua fursa ya kuuza umeme katika nchi jirani pamoja na kuongeza matumizi ya nishati katika shughuli za uzalishaji.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisema kukamilika kwa JNHPP ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Serikali yenye lengo la kuifanya nishati kuwa kichocheo cha uchumi.
Alisema kituo hicho kina mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 235, hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa taifa kukidhi mahitaji ya umeme kwa wananchi na sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, biashara na migodi.

“Ongezeko hili la uzalishaji limetuwezesha kuwa na ziada ya umeme na kuanza kutumia fursa hiyo kufanya biashara ya nishati na nchi jirani,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania tayari imeanza kuuza umeme kwa nchi ikiwemo Zambia na Kenya, huku ikiendelea na mazungumzo na mataifa mengine yenye mahitaji ya nishati.
Hata hivyo, alisema mafanikio ya JNHPP hayategemei uzalishaji pekee, bali pia uwezo wa kusafirisha umeme huo kwenda maeneo yenye mahitaji.

Alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji wa umeme, ikiwemo kukamilisha njia ya kusafirisha umeme ya Chalinze-Dodoma.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Dk Mostafa Kamal Madbouly, aliipongeza Tanzania kwa kukamilisha mradi huo mkubwa, akisema utekelezaji wake ndani ya miezi 42 kwa gharama ya takribani Dola za Marekani bilioni 2.9 umeonyesha uwezo wa kampuni za Misri kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati barani Afrika.
Madbouly alisema JNHPP pia umefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Misri, hasa katika maeneo ya uwekezaji, ujenzi, nishati, usafirishaji na kilimo.

Alisema mafanikio ya mradi huo yanapaswa kuwa kichocheo cha kuongeza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Naye Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina, alisema umeme unaozalishwa kupitia mradi huo unapaswa kutumika kama kichocheo cha kuvutia viwanda, biashara na ajira.
Alisema Tanzania ina nafasi ya kutumia uwekezaji huo kuunganisha miundombinu ya nishati na shughuli za kiuchumi ili wananchi wanufaike moja kwa moja.
Kukamilika kwa JNHPP kunatoa nafasi kwa Tanzania kuongeza uwezo wa kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa viwanda, biashara, madini, kilimo cha kisasa na huduma za kijamii.
Serikali pia inaendelea kuwekeza katika vyanzo mbalimbali vya nishati, ikiwemo maji, gesi asilia, jua, upepo na jotoardhi, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuimarisha uhakika wa nishati nchini.


