WATAHINIWA 1,168,649 WA DARASA LA SABA KUANZA MTIHANI KESHO

Na Aziza Masoud ,Dar es Salaam

BARAZA  la Mitihani la Tanzania (NECTA) limewataka watahiniwa 1,168,649 wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026 unaotarajiwa kuanza kesho kujiepusha na vitendo vya udanganyifu, huku wazazi, walezi na jamii wakitakiwa kuhakikisha mtihani huo unafanyika katika mazingira ya amani na utulivu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 8, 2026 Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Ally Mohamed  alisema mtihani huo unatarajiwa kufanyika kwa siku mbili, kuanzia  Septemba 9 hadi Septemba 10, 2026.

Alisema Jumla ya watahiniwa 1,168,649 wamesajiliwa kufanya mtihani huo, ambapo wavulana ni 531,467, sawa na asilimia 45.48, huku wasichana wakiwa 637,182, sawa na asilimia 54.52.

“Kati ya  watahiniwa 1,168,649 waliosajiliwa,watahiniwa  1,081,204 sawa na asilimia 92.52 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, wakati watahiniwa 87,445, sawa na asilimia 7.48, watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza,”alisema Profesa  Mohamed.

Alibainisha kuwa  watahiniwa 4,867 wenye mahitaji maalumu wamesajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwamo wasioona 82, wenye uoni hafifu 1,551, viziwi 999, wenye ulemavu wa akili 576 na wenye ulemavu mwingine wa muda mrefu 1,659.

“Mtihani wa mwaka huu utakuwa na masomo sita ambayo ni Kiswahili, Kiingereza Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi pamoja na Uraia na Maadili,”alisema Profes Mohamed.

Alisisitiza kuwa  mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi una umuhimu mkubwa kwa wanafunzi na jamii kwa jumla, kutokana na kuwa kipimo cha maarifa na ujuzi walioupata wanafunzi katika elimu ya msingi, sambamba na kuwabaini wenye uwezo wa kuendelea na elimu ya sekondari.

Alisema maandalizi kwa ajili ya mtihani huo yameshakamilika  ikiwemo  kusambaza kwa karatasi za mtihani pamoja na  nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Aidha aliongeza kuwa katika kuhakikisha mtihani unafanyika kwa haki na uadilifu,amewataka wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia mtihani huo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Baraza.

Pia amewakumbusha wasimamizi  wa mtihani huo kuhakikisha watahiniwa wote wanafanya mtihani kwa muda uliopangwa na katika hali ya utulivu, huku watahiniwa wenye mahitaji maalumu wakipewa haki zao za kufanya mtihani kwa mazingira yanayowezesha.

“Kwa watahiniwa wenye ulemavu, Baraza limeeleza kuwa wenye mahitaji maalumu watapatiwa muda wa ziada, ambapo wenye mahitaji yanayohusu Hisabati watapewa dakika 20 kwa kila saa, huku kwa masomo mengine wakiongezewa dakika 10 kwa kila saa, kulingana na maelekezo ya Baraza,”alisema Profesa Mohamed.

NECTA pia limewataka watahiniwa kuzingatia sheria na kanuni za mitihani, likisisitiza kuwa yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanafunzi wanapata mahitaji muhimu yanayowawezesha kufanya mtihani katika mazingira mazuri, huku wakikumbushwa kutowashirikisha katika vitendo vya udanganyifu.

“Baraza linatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi 2026 unafanyika kwa amani na utulivu,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ratiba rasmi ya NECTA inaonyesha mtihani wa mwaka 2026 utafanyika Septemba 9 na 10, ukiwa na masomo sita yanayofanyika katika siku hizo mbili.