Spika Zungu aipongeza Serikali kwa kufanya marekebisho kwenye baadhi ya tozo na kodi 

Na Benny Mwaipaja, Dodoma

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ameipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuimwagia maua yake kwa kukubali kwa dhati kufanyia marekebisho baadhi ya tozo na kodi mbalimbali zilizokuwa zinapendekezwa kufanyiwa marekebisho katika Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Mhe. Zungu amesema hayo leo tarehe 25 Juni, 2026, Bungeni Jijini Dodoma, wakati akihitimisha mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2026 uliopitishwa kwa kishindo na wabunge takriban wote.

Akihitimisha hoja hiyo itakayoiwezesha Serikali kukusanya na kutumia shilingi trlilioni 62.33, Mhe. Spika Zungu alimpongeza Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) wasaidizi wake, watendaji wa Wizara na wabunge wote kwa kujadili Muswada huo kizalendo zaidi kwa maslahi ya wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla.

“Waheshimiwa wabunge Muswada umesomwa kwa mara ya tatu na wabunge tumekamilisha kazi yetu na nichukue nafasi hii kuwapongeza sana imebaki hatua ya Mheshimiwa Rais ambaye atapelekewa Sheria hii ili aweze kuridhia ili iweze kufanyakazi” alisema Mhe. Zungu huku akishangiliwa na wabunge.

Alisema kuwa kulikuwa na vikao vingi vya majadiliano kati ya Bunge Kupitia Kamati yake ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Serikali ikakubali ndiyo maana Bunge lilikuwa na utulivu wakati wa kujadili Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka 2026/2027

“Na sababu Kuu ya Serikali kukubali ilikuwa ni kufuata na kujali maslahi mapana ya wananchi” Aliongeza Mhe. Zungu.

Aliyataja miongoni mwa maelekezo ya Serikali yaliyoridhiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ni pamoja na kuondoa kero ya wafanyabiashara ya kulipa kodi kabla hawajaanza biashara ambapo sasa wanaofungua biashara mpya wataruhusiwa kufanya biashara bila kulipa kodi kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuongeza kuwa huyo ndiye Rais anayejali maslahi ya wananchi wake.

Alisema kuwa Serikali imefuta pendekezo la kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye pikipiki baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia kutambua kuwa hivi sasa pikipiki ni chombo muhimu kwa maslahi ya Watanzania kufanya shughuli zao hususan vijana.

Mhe. Zungu alisema kuwa Serikali kupitia Ibara ya 9 (d)(i) imefanyia marekebisho kusudio la kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini kutoka asilimia 15 hadi asilimia 18 badala ya asilimia 20 iliyokuwa inapendekezwa kwa magari yenye umri wa miaka nane lakini hayazidi miaka kumi.

Alisema kuwa Serikali imeondoa pendekezo la kutoza kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia moja (1) kwenye malipo yanayohusu mazao ya kilimo, wanyama hai,
maziwa, Samaki, na mabondo kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye
Ibara ya 25 ya Muswada kwa kuwananchi wengi wanajihusisha na shughuli za kiuchumi Kupitia sekta hizo.

“Hivi sasa kuna mikataba 16 ya uchimbaji madini
kati ya hiyo, miradi tisa yenye thamani ya ya uwekezaji wa shilingi trilioni 9.9, iliyoweza kutekelezwa, lakini miradi hiyo ilikwama kutokana na vivutio vilivyotolewa kwenye mikataba ya msingi kutotambulika na Sheria za Kodi na kwamba mapendelezo yaliyotolewa yatakwenda kuifungua fursa za uwekezaji na kiuchumi na kutoa ajira kwa Watanzania ikizingatiwa pia kuwa Serikali inamiliki asilimia 16 ya hisa katika miradi hiyo.

Aidha, Mhe. Zungu alishauri Serikali kuendelea kubana matumizi yasiyo ya lazima ikiwemo ununuzi wa magari ya kifahari ili fedha hizo zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.

Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Seikali ya Mwaka wa Fedha 2026/2027, tarehe 11 Juni mwaka huu, Mhe. Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar alisema kuwa, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi trilioni 62.33 huku mapato yakitarajiwa kuwa shilingi trilioni 46.79, mapato ya kodi shilingi trilioni 36.99, na mapato mengine ni shilingi trilioni 9.24 (ikijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi trilioni 1.977) na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo shilingi bilioni 563.1.

Aidha aliongeza kuwa Ili kuendana na dhamira ya kujitegemea katika uendeshaji wa Serikali na maendeleo, takribani robo tatu ya bajeti yote ya mwaka 2026/27, sawa na asilimia 74.2 itagharamiwa na mapato ya ndani.

Matumizi na uwekezaji katika mali zisizo za kifedha yalikadiriwa kuwa shilingi trilioni 54.50 pasipo kujumuisha malipo ya mtaji wa deni la Serikali ambapo kati ya kiasi hicho, stahiki za watumishi ikijumuisha michango ya pensheni ni shilingi trilioni 10.13.

“Gharama za bidhaa na huduma itakuwa shilingi trilioni 5.22, malipo ya riba ni shilingi trilioni 6.86, ruzuku shilingi trilioni 25.32, mafao na misaada ya kijamii shilingi trilioni 1.01, uwekezaji katika mali zisizo za kifedha shilingi trilioni 2.33 na gharama nyingine shilingi trilioni 3.63.” alisema Mhe. Balozi Omar

Aliongeza kuwa kulingana na makadirio ya mapato na matumizi hayo, kunajitokeza nakisi kwenye bajeti ya shilingi trilioni 7.71 na Serikali itaendelea kugharamia nakisi ya bajeti hiyo kwa kutumia mikopo kutoka vyanzo vya ndani na nje kwa kuzingatia Mkakati wa Muda wa Kati wa Kusimamia Deni la Serikali (2025/26 – 2027/28).

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, Katika mwaka 2026/27, Serikali inatarajia kukopa jumla ya shilingi trilioni 15.54 ambapo kati ya kiasi hicho, mikopo ya ndani itakuwa shilingi trilioni 6.56, mikopo ya nje yenye masharti nafuu shilingi trilioni 6.55 na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 2.43.
Aidha, Serikali inakadiria kulipa malipo ya mtaji kwa mikopo iliyoiva shilingi trilioni 7.84.

Baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo na Bunge kwa kishindo, na kupitisha pia Muswada wa Shrria ya Fedha wa Mwaka 2026, sasa kinachosubiriwa ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiridhia na kuisaini Sheria hiyo ili iweze kutumika kuanzia tarehe Mosi Julai, 2026.