Na Asha Mwakyonde, RUKWA
TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imewahimiza vijana kutumia fursa za mafunzo, tafiti za afya na miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hiyo ili kuongeza ujuzi na uwezo wa kujiajiri au fursa za kuajiriwa.
Akizungumza leo tarehe 12 Oktoba, 2026 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NIMR katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika mkoani Rukwa, yenye kaulimbiu isemayo “Mazingira tofauti, fursa sawa kwa vijana.” Mtafiti Mwandamizi kutoka NIMR na Meneja wa Kituo cha Mbeya, Dk. Bariki Mtafya, amesema taasisi hiyo inatekeleza tafiti mbalimbali zinazolenga kuboresha afya za wananchi, zikiwemo tafiti za magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.

Amesema NIMR inatoa fursa kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali na wahitimu kushiriki mafunzo kwa vitendo na kufanya mazoezi katika shughuli za utafiti, hatua inayowasaidia kupata uzoefu na kujiandaa kuingia katika soko la ajira.
Dk.Mtafya ameeleza kuwa vijana wanaomaliza vyuo na ambao bado hawajapata ajira wanaweza kunufaika na fursa zinazopatikana kupitia miradi na shughuli za taasisi hiyo, ikiwemo kujifunza mbinu mbalimbali za kufanya tafiti za afya.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, vyuo na wadau wa sekta ya afya ni muhimu katika kuwajengea vijana uwezo na kuwafungulia njia za kushiriki katika shughuli za kitaaluma na maendeleo ya sekta hiyo.
Aidha, amesema NIMR inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya afya kupitia wataalamu wake, wakiwemo wataalamu wa sayansi ya jamii, madaktari na maabara kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu magonjwa na namna ya kuyadhibiti.
Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuzipa kipaumbele afya zao kwa kuwa ni msingi na mtaji muhimu wa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla hasa wakati huu ambao tunatekeleza dira ya maendeleo ya taifa ya 2050.
Katika eneo la utafiti na uzalishaji wa bidhaa za tiba asili, Dk. Mtafya ameeleza kuwa vijana wanaweza kunufaika na fursa zinazohusiana na upatikanaji wa malighafi, maandalizi ya bidhaa na shughuli nyingine zinazohusiana na miradi ya uzalishaji wa Tiba Asili kwa kutumia fursa zilizopo katika kituo chake cha Tiba Asili cha NIMR- Mabibo, Dar es Salaam.

Amesema taasisi hiyo pia hushiriki katika maonesho mbalimbali kwa kuonesha bidhaa zinazotokana na shughuli zake, zikiwemo bidhaa za tiba asili, ili wananchi waweze kuzifahamu na kupata maelezo sahihi ya namna ya kuzitumia na tafiti zinazoendelea.
Ameeleza kuwa tiba asili ina umuhimu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kiafya, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa bidhaa na ushauri wa wataalamu wa afya kabla ya kuzitumia.
Dk. Mtafya amewataka vijana wenye nia ya kujifunza na kushiriki katika sekta ya afya kutumia fursa za mafunzo, utafiti na miradi inayopatikana ili kujiongezea ujuzi, kukuza ubunifu na kuchangia maendeleo ya taifa.


